Jalang'o akana kuwa mmoja wa wanaume Diana Marua aliwahi chumbiana nao

Mbunge huyo alinyoosha maelezo kuhusu picha moja ya kitambo inayowaonyesha pamoja na Diana Marua, picha ambayo wanamitandao waliibua.

Muhtasari

• Nakumbuka kwamba picha lazima iwe ilipigwa kati ya miaka 10-15 katika karibu na duka la jumla la Jamia. - Jalang'o

Jalang'o ajitenga na madai ya kuwahi kuchumbiana na Diana Marua
Jalang'o ajitenga na madai ya kuwahi kuchumbiana na Diana Marua
Image: Instagram,Maktaba

Mwanasiasa Phelix Odiwuor amejitokeza wazi na kukana madai yanayomhusisha kuwa huenda alikuwa mmoja wa wanaume wenye pesa ambao mwanablogu Diana Marua alisema kwenye video yake kuwa alikuwa anachumbiana nao kabla ya kukutana na Bahati.

Baada ya video hiyo ya miaka miwili ikimuonesha Diana Marua akikiri kuwa maisha yake ya awali alikuwa anachumbiana na wanaume kadhaa wenye pesa ili kukidhi mahitaji yake, mashabiki na watumizi wa mitandao ya kijamii waliibua picha yake ya zamani akiwa na Jalang’o na kudai kuwa huenda ni mmoja wa wanaume hao wengi.

Ilimbidi mbunge huyo wa Lang’ata kuweka mambo wazi katika mahojiano na mwanablogu Mungai Eve ambapo alikana kabisa kuwa aliwahi kumchumbia Marua.

Alisema kwamba picha ambayo wanaonekana wakiwa pamoja ilikuwa ya kitambo sana kati ya miaka 10 hadi 15 na wamekuwa marafiki tu kwa muda mrefu ila hawakuwahi kuwa wapenzi kama ambavyo wanamitandao walikuwa wanasema.

“Nakumbuka kwamba picha lazima iwe ilipigwa kati ya miaka 10-15 katika karibu na duka la jumla la Jamia. Nadhani Diana alikuwa amekuja kununua nguo na tayari alikuwa superstar wakati huo. Aliomba picha nami nikapiga naye picha. Sijawahi kudate na Diana. Diana amekuwa rafiki yangu kwa muda mrefu na hata tulipopiga picha hiyo ilikuwa ni picha nzuri tu,” Jalang’o alinyoosha maelezo.

Kando na hayo, mchekeshaji huyo ambaye pia ni mtangazaji wa redio alisema hakuwa anajua Diana Marua anatrend mitandaoni kutokana na video yake ya miaka miwili iliyopita na kusema kuwa alijulishwa na rafiki yake mmoja na ndio akaenda pia kuitazama video ile.

Katika video hiyo, Marua alifichua kwamba maisha yake ya awali yalikuwa ni kiza tupu ambapo alilazimika kutafuta riziki katika mifuko ya wanaume wengi, baadhi waliokuwa katika ndoa kabla ya msanii Bahati ambaye ni mumewe kumnusuru kutoka katika maisha hayo ya dhiki.

Mpaka sasa, Diana na Bahati wana watoto watatu pamoja, wa tatu akiwa ni Malaika Bahati ambaye wamekaribisha takribani mwezi mmoja uliopita.