Ni mchungaji wa kweli, miujiza yake si vipindi - DJ Mo amtetea mkewe Size-8

Alisema kuwa kule Kibwezi Size 8 aliombea mtu ambaye hawakuwa wanajuana na akapata uponyaji.

Muhtasari

• Alisema kuwa ni kawaida watu kushuku miujiza ya watumishi wa Mungu kwani hajawahi ona miujiza ambayo inaaminiwa kuwa ya ukweli.

DJ Mo na mkewe Size 8
DJ Mo na mkewe Size 8
Image: Instagram

Kwa mara ya kwanza DJ Mo amejitokeza wazi na kumtetea mkewe Size 8 ambaye ni mchungaji na mwinjilisti.

Kwa muda sasa watu wamekuwa wa kutilia shaka maombi ya Size 8 ambapo amekuwa akionekana kuwaombea watu huku baadhi wakisema ni mitikasi ya mitandaoni na wengine wakisema kuwa maombi yake ni ya kinafiki wala si ya kweli kama anavyojiita mchungaji na mtumishi wa Mungu aliyetawazwa miaka michache iliyopita.

Akizungumza na mwanablogu Mungai Eve, DJ Mo alisema kuwa mkewe ni muombaji wa kweli na kutoa mfano kuwa maombi yake kwa mtu mmoja yalimponya kikweli na kuwa si mitikasi ya mitandaoni.

“Mimi ningekuwa nashangaa sana kama watu hawangemkejeli mke wangu. Vinginevyo, ningekuwa kama, ngoja mke wangu unafanya kitu kibaya. Ikiwa miujiza ni ya uwongo, basi ile ya kweli iko wapi? Sijawahi kuona mchungaji ambaye miujiza yake inaaminika. Nimekuwa naye na najua miujiza ni ya kweli sana. Nina furaha kwa sababu niko hapa kumuunga mkono. Nitamuunga mkono hadi mwisho,” DJ Mo alisema.

Mcheza santuri huyo wa muda mrefu aliwasuta wote wanaodhani kwamba Size 8 anatafuta kiki na neon la Mungu kuonekana akiwaombea watu na kufanya miujiza katika sehemu mbali mbali za nchi.

Alitolea mfano kwamba miezi michache iliyopita Size 8 alifanya muujiza eneo la Kibwezi alikokuwa anahubiri kwa kumuombea mtu mmoja ambaye hawakuwa wanajuana na akapona.

“Kuna madam alipona na hawajuani, alikuja hapo Kibwezi. Unajua mtu anaweza sema ilikuwa kipidni mlipanga, lakini yule hata hawakuwa wanajuana, alikuja akamuombea na ikawa hivyo, kwa hivyo wale watu ambao mnategemea kuwa hawatafanya miujiza hao ndio Mungu atatumia kufanya miujiza. Watu waache kusema ni vipindi, kuna wa ukweli na kuna si ya ukweli. Lakini wewe kama mhubiri fanya tu kile unafanya, Mungu ndiye atakulipa,” DJ Mo alisisitiza.