Ahsante kwa kuwa baba mwema kwa mtoto wetu - Nadia amwambia Arrow bwoy

Nadia Mukami alisema kuwa Arrow Boy amekuwa akimsaidia katika malezi ya mtoto wao

Muhtasari

• Kwenye Instagram Mukami alipakia video akimshukuru Arrow Boy kwa kuwa baba mzuri kwa mtoto wao.

• Mtoto wa wapenzi hao, Kai ambaye ni wa kiume amefikisha takriban miezi minane sasa tangu kuzaliwa.

Arrow Boy, Nadia Mukami na mtoto wao Kai
Image: Nadia Mukami Instagram

Mwanamuziki Nadia Mukami alimwandikia mpenzi wake Arrow Boy ujumbe huku akimsherehekea siku ya wanaume duniani.

Kwenye Instagram Mukami alipakia video akimshukuru mwanamuziki huyo kwa kuwa baba mzuri kwa mtoto wao.

"Kwa baba ya mtoto wangu almaarufu mpenzi wangu wa maisha ambaye hunisaidia kumlea mtoto wetu, Kai 22/7 haswa asubui kwa kuwa mimi si mtu wa kuamka mapema kabisa !! Asante," Nadia aliandika.

Nadia alizidi kumtakia mpenzi wake mema na kumpongeza kwa uwajibikaji wake.

Mtoto wa wapenzi hao wawili, Kai ambaye ni wa kiume amefikisha takriban miezi minane sasa tangu kuzaliwa.

Hivi majuzi, Mukami alipakia video ya kusherehekea mwanawe alipokuwa anafikisha miezi sita.

Alikuwa akicheza kwa mbwe mbwe huku Kai akiwa amefungwa kifuani mwake.

Mama huyo wa mtoto mmoja alikuwa anacheza kwa wimbo wake mpya ambao aliutoa mwezi wa Septemba akimshirikisha mpenzi wake Arrow Bwoy, wimbo kwa jina Kai Wangu.

“Mr Handsome ana miezi 6 😌♥️ Tuliamua kwenda kusherehekea nje ya Nairobi♥️🌺 Nakupenda sana mtoto wangu Kai, wewe ni furaha yangu na najivunia kuwa mama yako,” Nadia Mukami aliandika kwenye video hiyo.

Hivi majuzi Arrow Boy alikuwa anamsherehekea Nadia kwa siku yake ya kuzaliwa ambapo alimwandikia ujumbe.

"Ukaribu wetu unazidi Kuimarika Kila Siku. Mama wa ajabu kwa mwana wetu, mpenzi wa ajabu na rafiki , @nadia_mukami Nampenda mwanamke ambaye umekuwa ... Mwenyezi akujalie Kila la heri unapofikisha miaka 23 😁 heri njema ya kuzaliwa malkia wangu nakupenda," Arrow Bwoy alisema.

Wawili hao wamekuwa wakichumbiana kwa muda sasa baada ya Arrow Boy kumvalisha mama huyo pete ya uchumba.