Nilisherehekea mwaka mpya kwa nyumba kwa miaka mitatu - Jackie Matubia huku akizawadi wazazi wake nyumba

Matubia alieleza kuwa amekuwa akitamani kuwazawadi wazazi wake nyumba kwa miaka mitatu

Muhtasari

• Kwenye ukurasa wake wa YouTube, Matubia alieleza jinsi alivyokuwa na woga wakati wa kufanya maendeleo hayo.

• Matubia alieleza kuwa aliandika malengo yake mwanzoni mwa mwaka na malengo hayo yote yalitimia isipokuwa lengo la kuwanunulia wazazi wake nyumba.

Jackie Matubia
Image: Jackie Matubia Instagram

Mwigizaji Jackie Matubia amezungumzia suala la kuwazawadi wazazi wake na wadogo wake nyumba.

Kwenye ukurasa wake wa YouTube, Matubia alisema jinsi alivyokuwa na woga wakati wa kufanya maendeleo hayo.

Alieleza sababu yake ya kutofichua maendeleo yake kwenye mitandao na kusema kuwa amekuwa akisubiri kutimiza lengo lake la kuwazawadi wazazi wake nyumba.

"Kwa miaka mitatu iliyopita nimekuwa nikisherehekea mwaka mpya kwa nyumba,sikuwa na pesa na mwaka jana nilikuwa mjamzito," Matubia alieleza changamoto za kuwanunulia wazazi wake nyumba.

Mke huyo wa Blessing Lung'aho alisema kuwa aliandika malengo yake mwanzoni mwa mwaka na malengo hayo yote yalitimia isipokuwa lengo la kuwanunulia wazazi wake nyumba.

Baadhi ya malengo ambayo Matubia alitumainia kufanikiwa kufanya ni kama kuvalishwa pete ya uchumba, kupata mtoto na kuwa na nyumba ya kifahari.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kuwa aliposhindwa kuwanunulia wazazi wake nyumba kwa miaka miwili, alikuwa amehuzunika na kuvunjika moyo.

Matubia alieleza jinsi mume wake, Blessings Lung'aho alimpa nguvu kwa kumshauri na hata kwa kumtuliza alipohisi hayuko sawa.

"Nilikuwa kwenye giza, nilikuwa nimechoka. Namshukuru Mungu kwa kunipa mpenzi anayenielewa na aliyefahamu nilichokuwa ninataka sana maishani. Amekuwa akiniunga mkono nilipokuwa nikijiuliza maswali mengi," Matubia alieleza.

Aliendelea kusema kuwa hakutaka tu kuwanunulia nyumba bali pia alitaka kuwanunulia gari.

Alisema jinsi mambo mengi kama uchaguzi mkuu yalikuwa yakimzuia kununua nyumba ila hatimaye amefanikiwa kuwazawadi wazazi wake.

"Niliwasumbua wazazi wangu kitambo, unapofanikiwa, unafaa kuwalipa wazazi wako kwa yote waliyokufanyia, wape furaha," Muigizaji huyo alisema.