Harmonize athibitisha kutumbuiza tamasha la Sol Fest Desemba 17

Kikundi cha Sauti Sol kinaendelea kutoa orodha ya wasanii kadhaa watakaotumbuiza katika usiku huo wa tafrija kali la kufunga mwaka.

Muhtasari

• Sauti Sol walitangaza tamasha hilo lao kubwa kabisa la kila mwaka litafanyika Desemba 17 mwaka huu.

Harmonize kutumbuiza tamasha la Sol Fest
Harmonize kutumbuiza tamasha la Sol Fest
Image: Instagram

Msanii Harmonize kutoka lebo ya Konde Music Worldwide amedhibitisha kuwa atakuwa mmoja wa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha kubwa la kundi la Sauti Sol almaarufu Sol Fest litakalofanyika humu nchini mnao Desemba 17.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize alisema kuwa ni sharti ahudhurie kwani ameshapata mwaliko rasmi na kipindi hicho atakuwa humu nchini baada ya kutumbuiza katika tamasha la Eldoret.

“Niaje watu wangu wa 254 Kenya huyu ni Konde Boy kutoka Konde Music Worldwide na ninawadhibitishia kuwa nitakuwepo katika tamasha la Sol Fest mnamo Desemba 17. Ambia wenzako hili si la kukosa,” Harmonize alisema kwenye video fupi alipoipakia.

 Sauti Sol walitangaza tamasha hilo lao kubwa kabisa la kila mwaka litafanyika Desemba 17 mwaka huu na tayari wameanza kutoa orodha ya wasanii nguli kutoka bara la Afrika ambao watakuwa miongoni mwa watumbuizaji.

Sol Fest ni tamasha la kimuziki linaloandaliwa kila mwaka na kikundi cha wanamuziki cha Sauti Sol kama moja la kusherehekea mafaniko yao kimuziki kwa mwaka mzima na pia kutangaza maazimio yao katika mwaka unaofuata.