Nadia Mukami afichua sababu ya kutaka mtoto mwingine baada ya miaka 5

Nadia alisema malezi yamekuwa na changamoto ila anajikakamua

Muhtasari

• Akijibu maswali kwa Instagram, Nadia aliulizwa iwapo anapanga kumleta mtoto mwingine duniani hivi karibuni na kajibu...Labda baada ya miaka mitano, sitaki saa hii!

Nadia Mukami
Image: Nadia Mukami Instagram

Mwanamuziki Nadia Mukami amefichua kuwa hapangi kupata mtoto mwingine hivi karibuni.

Kwenye Instagram, mpenzi huyo wa Arrowboy aliulizwa iwapo anapanga kumleta mtoto mwingine duniani hivi karibuni.

"Tumtarajie mtoto wa pili hivi karibuni?" shabiki wake aliuliza.

Nadia alisema kuwa sasa hivi hana mipango ya kupata mtoto mwingine na kuwa anapanga kupata mtoto mwingine tena baada ya miaka mitano.

"Labda baada ya miaka mitano, sitaki saa hii! Eh ni kujitolea pakubwa sana," Mukami alisema.

Nadia pia alifichua kuwa mtoto wake, Kai  atafikisha miezi minane kesho.

Alieleza kwamba, kuwa mama halijakuwa jambo rahisi kwake kwani anajaribu kuwa mzazi bora na wakati huo huo kuzingatia taaluma yake ya muziki.

"Ni jambo kubwa sana, mambo ni mengi ya kufanya ila nimejaribu kadri ya uwezo wangu," Nadia alisema.

Hivi majuzi,siku ya wanaume duniani, kwenye Instagram Mukami alimsifia mpenzi wake ArrowBoy kwa kuwa mzazi anayemsaidia katika malezi ya mtoto wao.

Alipakia video akimshukuru mwanamuziki huyo kwa kuwa baba mzuri kwa mtoto wao.

"Kwa baba ya mtoto wangu almaarufu mpenzi wangu wa maisha ambaye hunisaidia kumlea mtoto wetu, Kai 22/7 haswa asubui kwa kuwa mimi si mtu wa kuamka mapema kabisa !! Asante," Nadia aliandika.

Imedhihirika, kupitia Instastory zake kuwa bila mume wake kumsaidia Nadia na malezi, angelemewa na kazi hizo kwani majukumu yake yamekuwa mengi.

Nadia na Arrow Boy wamekuwa wakichumbiana kwa muda sasa na kupata mtoto mmoja kwenye uhusiano wao.

Wawili hao wamekuwa wakishirikiana kumlea mtoto wao na hata kimuziki.

Waliachia wimbo mmoja unaoitwa 'Kai Wangu'  uliomsifia mtoto wao huku wakimkaribisha duniani na kumweleza jinsi wanampenda.