Alikiba, Harmonize, Rayvanny ni wasanii wakali - Diamond akiri

Diamond alisema kuwa wasanii wanafaa kuwa na umoja ili kuimarika kimataifa

Muhtasari

• Diamond alisema kuwa jambo linalowazuia wasanii wa Tanzania kuvuma hata kwa nchi za nje ni kuwa wana mazoea ya kushindana badala ya kuwa na umoja.

• Bosi huyo wa WCB alieleza pia kuwa mashabiki wakati mwingine huchangia pakubwa kwa muziki wa Tanzania kutovuma inavyofaa.

Diamond Platnumz
Image: Diamond Platnumz Instagram

Mwanamuziki wa Tanzania, Diamond amekiri kuwa wasanii wenzake wakiwemo Alikiba, Harmonize na Rayvanny ni wasanii wakali.

Diamond alisema kuwa jambo linalowazuia wasanii wa Tanzania kuvuma hata kwa nchi za nje ni kuwa wana mazoea ya kushindana badala ya kuwa na umoja.

Alieleza kuwa wasanii wanafaa kuwa na lengo la kusonga mbele wala si kubaki mahali pamoja wakizozana.

"Huku Tanzania tuna tabia ya kuonyeshana nani mkali kuliko mwenzake, hadi wa leo. Mpaka leo hamjafahamu kuwa nyote ni wakali tu? Hivi leo, nani asiyejua kuwa Alikiba ni msanii mkali, nani asiyejua Rayvanny ni msanii mkali, nani asiyejua Harmonize ni msanii mkali? Hivyo tushavipitisha vyote," Bosi huyo wa WCB alisema.

Diamond alisema kuwa hapendi kujihusisha na kitu ambacho watu wanazungumza kumhusu kwani anaweza kuwa mwenye mawazo na kujibu kwa madharau, jambo ambalo anafahamu litampotezea wakati.

Alilinganisha wasanii wa Tanzania na wa nchi za nje kama Marekani na kusema kuwa wasanii wa nchi yake wakizozana wale wa nchi za nje wanasonga na kuimarika kimuziki.

"Wasanii huongozwa na watu, marafiki,jamaa, lazima watuongoze kwenye njia ya kusonga mbele wala si chuki za wenyewe kwa wenyewe, kwa sababu zinaturudisha nyuma," Mondi alisema.

Alieleza pia kuwa mashabiki wakati mwingine huchangia pakubwa kwa muziki wa Tanzania kutovuma kama inavyofaa.

Diamond alisema kuwa yeye huielewa talanta yake vyema na hupenda kupuuzilia mbali wanaomsema vibaya.

"Huku Watanzania ukitoa nyimbo za kimataifa wanataka utoe nyimbo za lala salama, usipotoa wimbo wa kimataifa ni wa kwanza kukutusi, mashabiki pia huchangia. Nikitoa nyimbo, mimi huzima data ya simu, ukitaka kunitusi wewe tusi, sitambui," alisema.