Tiktoker akataa zawadi kwenye harusi yake, adai pesa kwenye bahasha

Mummie Francie alisema harusi yake ya kitamaduni itafanyika Busia Desemba 24 na kutoa masharti makali kwa watakaohudhuria.

Muhtasari

• Kama hilo halitoshi, wageni wake wanatarajiwa kuvalia maridadi, huku Bi Francie akisisitiza kuwa ni harusi, si sherehe ya mazishi.

Mummie Francie na mchumba wake
Mummie Francie na mchumba wake
Image: Instagram

Mwanatiktoker maarufu ambaye pia ni ‘makeup artist’ kutoka humu nchini Mummie Francie ametangaza kuwa harusi yake itafanyika rasmi Desemba 24, siku moja tu kabla ya sherehe za Krismas.

Kupitia video moja ambayo alipakia kwenye Tiktok yake, Mummie Francie amewaacha wengi katika mshangao mkubwa baada ya kutaja masharti makali kwa wale wote wanaotarajia kuhudhuria sherehe hiyo ya kufunga pingu za maisha na mchumba wake wa muda mrefu.

Sherehe ya harusi itafanyika katika kaunti ya Busia na inasemekana kuwa itakuwa ni harusi ya kitamaduni inayoambanata na masharti mengi ya kushangaza kwa watakaohudhuria.

Katika video hiyo ya TikTok, alianza kwa kusema kwamba kwa ajili ya harusi yake, lazima apate michango, na kiasi ambacho wageni watatoa kitalingana na chakula wanachokula.

"Kwa nini nijitahidi lakini najua kuwa mfuko wangu unaweza kulisha watu wawili tu? Wachungaji wanaosimamia kufunga ndoa yangu. Usifikiri kwamba utachangia Sh100 na kupata sahani iliyojaa nyama kama mtu aliyechangia Sh1000,” Francie alisema katika kile kilionekana kama ni onyo kali.

Kama hilo halitoshi, wageni wake wanatarajiwa kuvalia maridadi, huku Bi Francie akisisitiza kuwa ni harusi, si sherehe ya mazishi na kusema hataki zawadi bali anataka pesa zilizowekwa ndani ya bahasha kama zawadi maalum.

“Usiniletee zawadi. Weka pesa zako kwenye bahasha. Ukipuuza ushauri huu na uje na friji yako nitauza hapohapo. Hata ukiniletea picha yangu, nitaiuza," alisema.

Mwanatiktoker huyo hajawasaza wale wenye midomo kaya ya kuwasema watu hovyo. Ameahidi kuwa kama unajua utahudhuria sherehe yake, basi umbea wako na udaku wote uuache ndani kwako kabla kutoka kwani atakuwa na vinasa sauti vya siri katika kila kiti na ole wako ukimsengenya.

“Vipaza sauti vitaunganishwa na spika kwa hivyo thubutu kuja na kunisengenya kwa mdomo mbaya kwenye harusi yangu mwenyewe. Nitafanya dhamira yangu kukuaibisha kwa kipimo kile kile.”

“Pamoja na familia zao, Mummie na Andy wanakualika kusherehekea harusi yao ya kitamaduni tarehe 24 Desemba, katika Kijiji cha Namutsula, mji wa Matayos, Kaunti ya Busia. Mandhari yatakuwa nyeusi na mguso wa dhahabu. Zawadi kwenye bahasha zinapendekezwa sana.” Tangazo la harusi hiyo linasoma kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.