Maoni: Hakuna Rayvanny bila Diamond, ndio maana anadumisha urafiki na WCB Wasafi

Msanii huyo tangu kujiunga na WCB, ameshirikiana na Diamond kwa collabo 10, zaidi ya msanii yeyote ukanda wa East Afrika.

Muhtasari

• Hivi majuzi wawili hao wameachia collabo yao ya ngoma ‘Nitongoze’ ambayo ni ya 10 ndani ya miaka 6 tangu kujuana – rekodi ambayo haijawahi kuonekana na wasanii wengine.

Diamond na Rayvanny
Diamond na Rayvanny
Image: Instagram

Kwa muda mrefu, wadau wa muziki hasa wa Bongo Fleva wamekuwa wakilonga kuwa baadhi ya wasanii wanapoondoka lebo ya Wasafi basi ni kama ndio mwanzo wa kujichimbia makaburi yao wenyewe.

Wengine wanahoji kuwa hii ndio sababu kuu ya msanii Rayvanny kuendelea kudumisha urafiki na ukaribu wake na lebo hiyo hata baada ya kuondoka miezi kadhaa iliyopita ambapo alianzisha lebo yake ya Next Level Music.

Hivi ni kweli kuwa Rayvanny akianzisha bifu na Diamond atakuwa ndio anaelekea gizani katika taaluma yake ya kimuziki?

Msanii huyo aliingia katika lebo ya WCB Wasafi mwaka 2015 na mpaka kuondoka kwake 2022, amekuwa msanii ambaye amefanya collabo nyingi zaidi ya bosi wake Diamond Platnumz.

Hivi majuzi wawili hao wameachia collabo yao ya ngoma ‘Nitongoze’ ambayo ni ya 10 ndani ya miaka 6 tangu kujuana – rekodi ambayo haijawahi kuonekana na wasanii wengine.

Huu ni wimbo wa kwanza kwa Rayvanny kumshirikisha Diamond akiwa nje ya WCB Wasafi lakini ni wimbo wa nane kufanya pamoja (wawili pekee) tangu mwaka 2016 walipotoa wimbo wao wa kwanza, Salome.

Rayvanny na Diamond wameshirikiana kwenye nyimbo kama Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Vumbi, Amaboko na Woza, huku wakiwa wamekutana kwenye ngoma mbili za wasanii wote wa WCB, ‘Zilipendwa na Quarantine’, hivyo kufanya jumla ya nyimbo 10.

Katika nyimbo hizo nane, Diamond amemshirikisha Rayvanny katika nyimbo zake mbili, Salome na Iyena, huku Rayvanny akimshirikisha Diamond kwenye nyimbo sita ambazo ni; Mwanza, Tetema, Woza, Timua Vumbi, Amaboko na Nitongoze.

Kutokana na ukaribu wake huu na bosi wake, wengi wanahisi msanii huyo huenda anajua kile kitakachomkabili pindi atakapokinukisha baina yake na Diamond.

Kwa mfano wa haraka tu, Rayvanny alitoa collabo yake ya kwanza nje ya Wasafi na msanii kutoka Albania, Luana Vjollca kwa jina Pele Pele, ngoma ambayo haikufanay vizuri kama wengi walivyokuwa wanatarajia.

Ngoma hiyo ambayo ina zaidi ya miezi mine tangu kutoka ina watazamaji milioni 1.6 tu huku ile ya Nitongoze ambayo wameachia wiki chache zilizopita akimshirikisha Diamond ikiwa imeipiku kwa kupata watazamaji milioni 2.

Hili ni dhibitisho tosha kuwa msanii Rayvanny hawezi kusababisha pakubwa akijitenga na Diamond na ndio maana ameendeleza ukaribu wake na Simba huyo wa Tandale.