Kambua amtambulisha binti yake mrembo mwezi mmoja baada ya kuzaliwa (+video)

Msanii huyo alidokeza kuwa bintiye alizaliwa mwezi mmoja uliopita.

Muhtasari

•Kambua alichapisha video inayoonyesha akiwa amemkumbatia binti yake mchanga na kufichua kwamba amempatia jina Nathalie Nyacira Mathu.

•Kambua alibainisha kuwa anajivunia sana kuwa mama ya mtoto huyo.

Siku moja tu baada ya kutangaza ujauzito wake wa tatu, mwimbaji wa nyimbo za injili Kambua Manundu amefichua kuwa tayari amejifungua.

Jumanne, mwanamuziki  huyo mrembo alichapisha video inayoonyesha akiwa amemkumbatia binti yake mchanga na kufichua kwamba amempatia jina Nathalie Nyacira Mathu. Alidokeza kuwa bintiye alizaliwa mwezi  mmoja uliopita.

"Nathalie Nyacira Muthiga Mathu. Msichana mrembo zaidi ambaye nimewahi kuona kwa macho yangu, ana roho ya upole. Mwezi mmoja ambao umepita umekuwa wa thamani sana kwangu, upinde wangu wa mvua," alisema kupitia Instagram.

Kambua alibainisha kuwa anajivunia sana kuwa mama ya mtoto huyo.

Alisema baraka ya mtoto huyo ni fidia kutoka kwa Maulana baada ya kumpoteza mwanawe mwaka uliopita.

"Mungu wangu- fidia yangu kubwa na iliyopita; Asante kwa kutubariki. Mungu wa Kambua, asante kwa kubaki mkweli kwa jinsi ulivyo. Kwa Yale yote umetenda, niruhusu nitoe shukurani 🦋," alisema.

Mwimbaji huyi aliambatanisha ujumbe huo na video ya  mkusanyiko wa matukio kadhaa tangu kuzaliwa kwa Nathalie.

Kambua alifichua ujauzito wake siku ya Jumatatu. Wakati akitangaza habari hizo, mwimbaji huyo alikukumbuka masaibu yaliyomkumba mwaka jana alipopoteza mwanawe siku chache baada ya kujifungua.

"Zaidi ya mwaka mmoja uliopita nilimshika mwanangu wa thamani mikononi mwangu huku mwili wake mdogo ukipoa. Nilimezwa na giza nene, nene. Nilipata kujua huzuni ambayo sikujua inawezekana. Lakini Mungu alikaa nami katika giza langu. Na polepole akaanza kuninyanyua.

Alinikumbusha pia kwamba miaka iliyopita nilipokea ripoti ya daktari iliyosema siwezi kamwe kupata watoto. Alinikumbusha kwamba wakati ulimwengu ukinidhihaki alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya wema wangu na utukufu wake," alisema.

Kambua pia alitumia fursa hiyo kuwatia moyo wanawake wenye matatizo ya kupata watoto na waliopoteza ujauzito.