Tutafunga harusi mwaka ujao na mpenzi wangu wa miaka 3 - Stevo Simple Boy

Alishangaza wengi aliposema kuwa amekuwa kwenye uhusiano na mwanamke mmoja kwa jina Grace Atieno kwa miaka 3 iliyopita.

Muhtasari

• Mwaka ujao, hio itakuwa ndoa ya faragha, nitafanya harusi hivi ndio watu watajua nina mke - Simple Boy.

• Alisema kuwa hawezi rudiana tena na Pritty Vishy.

Msanii Stevo Simple amezungumzia kwa hisia kali himizo la wimbo wake mpya
Msanii Stevo Simple amezungumzia kwa hisia kali himizo la wimbo wake mpya
Image: instagram

Mwanamuziki Stevo Simple Boy amefunguka kuwa kwa sasa yupo kweney mahusiano na mtoto mmoja wa Kiluo kwa jina Grace Atieno.

Msanii huyo wa Freshi Barida alifichua haya akizungumza kwenye blogu ya mtangazaji Mwende Macharia. Alisema kuwa anampenda sana mwanadada huyo na mwaka kesho wanatarajia kufunga ndoa rasmi.

Simple Boy ambaye ana miaka 32 alisema kuwa wamechumbiana na mwanadada huyo kwa muda mrefu sana wa zaidi ya miaka 3 na mwakani watahitimisha uchumba na kutulia kama wanandoa.

Niko na jiko na ametulia tu. Ni wa kitambo, wa miaka mitatu iliyopita. Unajua wanasema mwanamke si gongingo wala si sefu, bali ni tabia heshima na maadili mema. Mimi niliangalia maadalili mema kwa huyo msichana, na nikasema kama uko serious kunipenda, nami pia nitakuwa mwaminifu kwako. Sasa napanga kuenda kuona wazazi wake,” Simple Boy alimwambia Mwende.

Jibu hili liliwashangaza wengi ambao wanakumbuka kuwa msanii huyo mapema mwaka huu ndio alimaliza uhusiano wake na Pritty Vishy ambaye alisema ndiye alikuwa mpenzi wake wa pekee, lakini kusema kuwa ana mpenzi wa miaka 3 kunakinzana kwa kiasi kikubwa na tamko hilo la awali.

Hivi karibuni, alionekana na mwanamke mwingine kwa jina Gee ambaye hata walitoa wimbo wa harusi na yeye wakiigiza kuwa wako katika mapenzi kumbe baadae ikaja kufahamika ni kiki tu ya mitandaoni walikuwa wanafukuzia.

Simple Boy akilizungumzia hilo, alisema kwamba amefika mwisho wa kufukuzia kiki mitandaoni na badala yake sasa mwakani atatulia katika ndoa.

“Mwaka ujao, hio itakuwa ndoa ya faragha, nitafanya harusi hivi ndio watu watajua nina mke. Ukiweka mpenzi wako kwenye mitandao ya kijamii, sana sana mabinti, kuna kitu fulani ndani yao, kiburi sasa inaanzia hapo. Sasa anaanza, 'Stivo hanifai, nataka yule akona mali, maji yikisha mwagika ndio anajua,” alisema.

Alidhibitisha kuwa hawezi rudiana na aliyekuwa mpenzi wake, Pritty Vishy huku akisema kuwa kitonga sasa kiko kwa mtoto mmoja tu kwa jina Grace.

“Kwa sasa hivi ni mmoja. Si Pritty, ni Grace. Kwa maisha yangu. Hao wengine ni baragoi tu. Hao wengine ni kukuja kumegemege na kusepa.”