Akothee afurahia kupata hati miliki ya shule yake 'Akothee Foundation Academy'

Mapema mwaka huu Akothee alisema ndoto yake ni kufungua shule ya kuwapa watu angalau elimu ya kujua kusoma na kuandika.

Muhtasari

• Hebu wazia jamii ambayo watoto wanaweza kupata ELIMU BURE, Angalau kusoma na kuandika - Akothee aliandika.

Akothee akionesha hati miliki ya shule yake
Akothee akionesha hati miliki ya shule yake
Image: Instagram

Mwanamuziki na mjasiriamali Akothee hatimaye ametangaza kupata hatimiliki ya shamba ambalo anakusudia kujenga shule kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa watuwasiojiweza kupata elimu.

Kupitia Instagram yake, Akothee alipakia picha akiwa ameshikilia hatimiliki hiyo pamoja na mchumba wake mzungu na kusema kwamba hatimaye ndoto yake ya kuanzisha shule kwa ajili ya kuwakimu watoto wa maskini kielimu itafanikishwa.

“Hatimaye Tulipata Hati miliki ya The great Akothee foundation Academy. Imetolewa na si mwingine ila Mwanzilishi Miss ESTHER AKOTH KOKEYO. Wacha kazi ianze,” Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye utajiri wa aina yake alitangaza mapema mwaka huu kwamba pindi hajafikisha miaka 45, atahakikisha ameacha kitu kitakacholeta tija kwenye jamii yake na ambacho kitamfanya kukumbukwa kama mtu aliyepambania vizazi vingi.

Alisema kuwa ndoto yake kubwa ni kujenga shule ya kutoa angalau elimu ya msingi ya kujua kusoma na kuandika kwa watu wa jamii yake ambao hawana uwezo wa kuipata elimu kutokana na gharama ya juu.

Awali, Akothee aliweka wazi kuwa shule hiyo yake ingeanza kutoa huduma kwa watoto kuanzia Februari mwaka ujao, huku akipakia bendera ya shule yenyewe.

“Hebu wazia jamii ambayo watoto wanaweza kupata ELIMU BURE, Angalau kusoma na kuandika. Mwishoni mwa mwaka jana nilitoa ekari 7 za Ardhi kwa AKOTHEE FOUNDATION. Akothee foundation Academy iko njiani. Nikizungumza, nafanya. Hii ndio ndoto kuu inayonisababishia kukosa usingizi usiku. Kuvunja ardhi 10. Januari 2023. Akothee Foundation Academy. Kutoa elimu bure kwa watu wasiojiweza. Wanafunzi wataoga shuleni, watavaa shuleni, watakula kiamsha kinywa na chakula cha mchana shuleni,” msanii huyo aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii.