Ndoto yangu ni kushinda Oscars Award mamangu akiona - Crazy Kennar

Mcheshi huyo alimtakia mamake maisha marefu ili kushuhudia akituzwa tuzo ya kifahari katika malimwengu ya uigizaji, Oscars Award.

Muhtasari

• Kwa sasa Kennar ni balozi wa kujitolea kupigana vita na msongo wa mawazo na unyongovu.

Mcheshi Crazy Kennar na mamake
Mcheshi Crazy Kennar na mamake
Image: Instagram

Mchekeshaji Crazy Kennar kwa mara ya kwanza kwa muda mrefu amepakia picha ya pamoja na mamake kwenye instastoory yake.

Kennar ambaye alionekana kulandana na mamake shilingi kwa ya pili alitoa ujumbe ambao kila mtoto anaomba siku zote kwa wazazi wake na pia kila mzazi anamuombea mtoto wake.

Wazazi wengi wanataka kuishi na kushuhudia mafanikio ya wanawe kwani hakuna mtu anayeamini katika ndoto za mtoto kama mzazi wake – shabiki wake nambari moja.

Na pia kila mtoto anaomba wazazi wake kuwa hai ili kuwalipa faraja kwa kumpa matunzo na malezi bora maishani.

Kwa Kennar, hali si tofuati kwani ombi lake kuu ni mamake kuwa hai na mwenye afya tele hadi pale kijana wake atapanda kwenye jukwaa kubwa kabisa duniani na kushinda tuzo bora duniani katika fani ya uigizaji – Oscars Award.

“Lazima aishi mpaka pale atakapomshuhudia kijana wake akishinda Oscars,” Crazy Kennar aliandika.

 Kennar ni mwigizaji wa skits za kuchekesha mitandaoni ambaye kupitia mitikasi hiyo, amepata ufanisi mkubwa mpaka kutembea kote duniani.

Wiki kadhaa zilizopita, alikuwa nchini Uingereza katika kongamano la wakuza maudhui wachanga mitandaoni ambapo alikutana na binadamu mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mtandao wa TikTok, Khaby, raia wa Senegali ambaye sasa ana makazi yake nchini Italia.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa ni balozi wa kutoa hamasisho kuhusu jinsi watu wanaweza wakashinda msongo wa mawazo na unyongovu.

Pia ni mmiliki wa mgahawa wa chakula kwa jina Instant Delicacies.