Nicah the Queen: Ndoa yangu itadumu na nitashangaza wengi

Mnaosema ndoa yangu itafeli, Ninaandika haya ili kubatilisha Maneno yenu katika Jina Kuu la Yesu - Nicah.

Muhtasari

• Alisema kuwa wanaomsema kwa njia hiyo ni kwa sababu ni mwanamke huku akiuliza mbona hawakumsema Ofweneke alipooa.

Wapenzi DJ Slahver na Nicah the Queen
Wapenzi DJ Slahver na Nicah the Queen
Image: Instagram

Msanii wa injili Nicah the Qeen amevimbia blogu moja ya humu nchini iliyochapisha kuwa ndoa yake ya mchezxa santuri DJ Slahver haitadumu.

Blogu hiyo ilichapisha hadithi hiyo siku moja tu baada ya msanii huyo kupakia picha akionesha kuwa mpenzi wake DJ Slahver hatimaye alimvisha pete ya uchumba katika tafrija ya nyumbani ambayo alimfanyia kama surprise kwa kushirikiana na wanawe wawili.

Nicah ambaye aliandika ujumbe mrefu wenye ghadhabu alisema kuwa ni wazi mwenye kuchapisha kuwa ndoa yake haitadumu ana tatizo la kibinafsi na yeye huku akionya watu dhidi ya kuandika habari zake ovyo.

Msanii huyo pia alisema kuwa wanaodhihaki uhusiano wake mpya baada ya kutengana na mchekeshaji Dr Ofweneke ni wale wanaomuonea kutokana labda na jinsia yake na nia yao ni kumporomosha tu kwa misingi ya jinsia.

“Ni wazi kwamba aliyeandika makala hii ana tatizo nami….acha niwape uhondo wote! Nilitengana na Ofweneke kwa miaka 6! Alioa ndani ya mwaka wa kwanza wa kuachana kwetu lakini sikuwahi kuwaona nyinyi mkiandika juu yake! Lakini sasa kwa vile ni mwanamke ambaye amepona na kuendelea na watoto wake wawili wazuri na Mungu amenikumbuka na kunibariki kwa mwanaume anayeupendeza moyo wake mna la kusema! Ninaandika haya ili kubatilisha Maneno yenu katika Jina Kuu la Yesu!” Nicah alisema.

Alizidi kukemea hao wanaosema kuwa ndoa yake haitadumu huku akisema kuwa watashangaa sana wakiona anadumu kwenye ndoa na DJ Slahver.

“Na ninaamuru na kutangaza kwamba nitafurahia mume wangu na ndoa yangu! Nitaleta ripoti nzuri kuhusu jinsi ndoa inavyofanya kazi! Mungu amenipa sura mpya ya kufafanua upya ndoa na uhusiano kwa watoto wangu…Wako karibu kuona jambo zuri ambalo litawaathiri na mawazo yao kuhusu ndoa. ITAFANYA KAZI NA @slahverdon na NITAENDELEA KUIFANYA KAZI MPAKA ITAKAPOFANYA! NITAWASHTUA!” alisema.

Pia alimalizia kwa kuwapa moyo kina mama ambao wanaishi bila wanaume huku akiwaambia kuwa ipo siku.

“Wadada warembo wote waliopo nje Mungu awarudishe na akishafanya watakuwa na wivu sana wanaweza kuandika tu chochote.”