Usinywe pombe mbele ya watoto wako, Usiende baa na mkeo - mwandishi Silas Nyancwani

Pia alishauri wazazi kutokunywa pombe karibu na watoto wao haswa msimu huu wa Krismasi.

Muhtasari

• Aliwashauri wanaume kuchukua jukumu la kuongoza familia kwa njia sahihi huku akisema hakuna ushujaa katika ulevi kwa mwanaume.

• Aliwashauri wazazi wote kutokuja na pombe nyumbani au hata kuionyesha kwa watoto wao.

Mwandishi wa Memo za ushauri kwa wanaume, Silas Nyanchwani.
Mwandishi wa Memo za ushauri kwa wanaume, Silas Nyanchwani.
Image: Maktaba

Mwandishi Silas Nyanchwani Gisiora ametoa ushauri kwa wazazi jinsi ya kuweka heshima kati yao na watoto wao haswa msimu huu wa Krismas wenye sherehe nyingi za kila aina.

Ushauri wake haswa uliwalenga wale wanaopenda kutumia vileo na kuwaambia kuwa wasifanya udhubutu hata sekunde moja wa kuandamana na wanao kwenda sehemu za burudani kama vilabu vya kuuza pombe.

Mwandishi huyo alisema kuwa alipigwa na butwaa baada ya kuona wanawake katika klabu moja wakiwa wanakunywa pombe kando ya watoto wao wadogo, jambo ambalo lilimkarifisha mno.

“Nilipitia sehemu moja ya burudani na kupata wazazi wachanga walio na watoto, wengine kama wachanga, wakiendelea kunyonyesha, ndani. Sio katika sehemu ya nje ya kilabu ambapo wakati mwingine watoto hujumuika. Walikuwa ndani kabisa ya klabu. Watoto wakila chips na sausage mbele ya chupa mbaya za vileo,” Nyanchwani alisema.

Alitumia nafasi hiyo kutoa ushauri kwa wenye hulka ya kulewa haswa wanaume na kuwausia wasiwahi fanya makossa ya kuandamana hata na wake zao kuenda kulewa kwani hivyo ndivyo heshima katika ndoa hupotea.

“Msifanye hivyo jamani. Acha kuwapeleka watoto mahali ambapo pombe hutolewa. Kwa wanaume hapa acheni kukaa na wake zenu na watoto kwenye baa. Usinywe pombe mbele ya watoto wako. Usiende baa na mkeo. Unaweza kukaa naye mara moja au mbili kila baada ya miaka kumi, lakini hakika si kila siku,” Mwandishi huyo alishauri.

Pia aliwashauri waraibu kukoma kabisa kuleta pombe nyumbani au hata kuiweka kwenye rafu za nyumbani ambapo watoto wanaona kwani hivyo ni kama kuwafunza tabia ya kujisemesha kuwa wakiwa watu wazima wataiga tabia kama hiyo.

Pia alisema kuwa mlevi mbele ya watoto wako ni kuchora taswira hasi vichwani mwao kwani mtu ukiwa mlevi unaonekana kama kinyago kisichoridhiki.

“Usiwe mlevi karibu na watoto wako. Hii inatumika kwa wanaume na wanawake. Hakuna kitu kinachopiga kelele za kutowajibika kama mzazi aliye na hangover. Kwa wanaume hapa, unapaswa kuwa shujaa kwa mke wako na watoto. Hakuna kitu cha kishujaa katika ulevi. Pombe hukufanya uwe hatarini ikiwa huwezi kuidhibiti.”