Maua si zawadi katika mwaliko wa harusi, mtu ametumia pesa nyingi - Anerlisa Muigai

Muigai aliwataka watu kuzoea kubeba zawadi angalau kuanzia mwaka huu.

Muhtasari

• Anerlisa amewahi kuwa katika ndoa na kufanya harusi, wengi walihisi kitu alichokuwa anakizungumzia ni kile alichopitia katika harusi yake na Ben Pol.

Amerlisa Muigai asema maua si zawadi katika harusi
Amerlisa Muigai asema maua si zawadi katika harusi
Image: instagram

Mrithi wa kampuni ya kutengeneza vileo ya Keroche, Anerlisa Muigai amewasuta watu ambao wanapewa mialiko kuhudhuria harusi halafu wanajitokeza mikono mitupu bila zawadi yoyote.

Muigai alisema kuwa katika uchumi wa sasa mtu unapopewa mwaliko wa harusi, hufai kujitoma mikono mitupu kwani haitarambwa.

Pia hakuwasaza wale ambao wanajibebesha maua akisema kuwa ingawa wengi wamekuwa wakidhani maua ni zawadi tangu miaka ya zamani lakini ukweli ni kwamba maua si zawadi na hayana thamani yoyote.

Alishindwa kuelewa ni kwa nini wengi wanaopata mialiko hiyo hujiwasilisha mikono mitupu wakiwa wanatarajia kuona maandalizi mazuri na vyakula vya hadhi ya nyota tano, bila kujua kuwa mwenye shughuli amegharamika pakubwa.

“Sijawahi elewa ni kwa nini watu wakialikwa katika hafla za kusherehekea siku ya kuzaliwa au harusi huwa wanaenda mikono mitupu bila zawadi. Maua si zawadi. Namaanisha kuwa mtu huwa ametumia gharama nyingi sana kufanikisha shughuli hiyo, lakini bila aibu wewe unaenda tu mikono mitupu, kweli?” Anerlisa aliuliza.

Wengi walihisi mwanadada huyo ana uzoefu kwa kile alichokuwa akikikashfu kwani amewahi kuwa mwenye harusi wakati mmoja japo haikudumu.

Ikumbukwe miaka miwili iliyopita Arnelisa alifunga harusi ya Kanisa na mwanamuziki kutoka Tanzania, Ben Pol, japo ndoa yao ilisambaratika miezi michache baadae na akarudi Kenya.

Tangu kuachana na Pol, Anerlisa alidokeza kuwa yuko katika mahusiano lakini hajawahi muonesha sura mpenzi huyo wake mpya, na wengine wakidai kuwa uhusiano huo pia haukudumu sana na sasa yupo bila mpenzi.

Kupitia instastory yake, Anerlisa baada ya kutoa mzomo huo, alipakia maandishi mengine ambayo kwa kiasi fulani yanadokeza kuwa huenda bado hajapata mpenzi na yuko katika harakati ya kupata mmoja.

Maandishi hayo yalisema kuwa katika harakati ya kutafuta mpenzi, atakuwa na utaratibu wa aina yake kumchagua mtu ambaye atampa muda na moyo wake kwani amechoka kuchezewa.

“Mimi ni mtu wa kuchagua kwa kuzingatia mambo mengi katika yule ambaye nitamuelekezea nguvu zangu. Napendelea kuhifadhi wakati wangu, nguvu na roho kwa pekee kwa yule anayeonyesha uaminifu,” Anerlisa alidokeza.