Mwanzo mpya 2023: Jimal aomba msamaha kwa Mungu, atarajia kupata mke mpya

Jmal alishambuliwa vikali na wanamitandao waliomsuta kwa kutoa ushauri wa ndoa hali ya kuwa yake ilimtokea puani.

Muhtasari

• Mfanyibiashara huyo aliwashauri wanaume kuoa wanawake ambao wanawaombea badala ya kuchokora simu zao.

• Pia aliomba radhi kwa Mungu huku akidokeza kuwa huenda mwaka huu akajaribu karata katika bwawa la mapenzi.

Jimal Rohosafi, mfanyibiashara.
Jimal Rohosafi, mfanyibiashara.
Image: Instagram

Mfanyibiashara Jimal Rohosafi ameamua kuanza mwaka kwa kutubu dhambi zake zote ambazo ziliona maisha yake katika jungu la mapenzi yakikumbwa na misukosuko na kimbunga kikali.

Kupitia instastories zake, Jimal alionekana kutubu kwa Mungu huku akijiombea mwaka mpya 2023 kuwa na mabadiliko mapya katika maisha yake na kumsihi Mungu kutokubali dhambi zake kufungia mafanikio yake.

“Mungu jamani usiruhusu dhambi zangu kufungia mafanikio na Baraka zangu. Tafahali naomba unisamehe. Mwaka mpya wa mabadiliko 2023,” Jimal aliandika.

Jimal mwenye kismati cha faida kibiashara bila bahati katika mapenzi alitumia fursa hiyo pia kutoa ushauri kwa wote ambao wanatarajia kuingia katika ndoa mwaka huu.

Kulingana na Jimal, mwanaume yeyote anayetaka kufanikiwa katika ndoa anafaa kuzingatia kumtafuta mwanamke atakayemwekea mikono kichwani wakati amelala na kumkuombea na si yule anayekimbilia kudukua simu ya mumewe wakati amelala.

“Oa mwakamke ambaye kwa siri atakuwekea mikono kichwani na kukuombea wakati umelala na si yule anayekimbilia kuchokonoa simu yako,” Jimal alisema.

Jimal kutoa ushauri wa ndoa ni kama kinaya kwani ndoa zake mbili zilimtokea puani mwaka jana ambapo mke wa kwanza Amira alimbwaga baada ya kuanza uhusiano wa kimapenzi na mwanasosholaiti Amber Ray.

Uhusiano wake na Ray pia haukusubiri kuchanua. Alimbwaga na kuifuta tattoo yake mgongoni na tangia hapo Jimal amekuwa akionekana mwenye kuteseka kimapenzi mpaka wakati mmoja kuamua kumeza kiburi na kumuandiki ujumbe wa hadharani mkewe Amira akimuomba radhi na kutaka warudiane kwa ajili ya kulea watoto.

Amira ambaye alionekana bado kutopona jeraha la maumivu aliyopata baada ya Jimal kumwendea Amber Ray alikakaa kata kata msamaha huo. Kwa upande mwingine Amber Ray alisonga mbele na maisha yake ambapo hivi sasa ni mchumba wa mtu baada ya kuvishwa pete ya uchumba na Kennedy Rapudo.

Jimal akiwa kama mtu aliyebaki kwenye mataa Asijue be wala te, ameamua kurudi kwenye mitandao ya kijamii kuhubiri kuhusu ndoa na uhusiano, licha ya kushindwa kushika hatamu za uongozi katika ndoa yake iliyoingia mchangani.