Syokau: Sikusema namtaka Ringtone, nilikuwa nataka tu maisha ya Runda na pesa zake

Justina alisema bado ombi lake mwaka 2023 ni kupata mwanaume tajiri.

Muhtasari

• Mimi kusema kuwa nilikuwa namtamani kimapenzi Ringtone haikuwa na maana kuwa ni yeye, nilikuwa natamani Runda - Syokau.

Wasanii wa injili Ringtone na Justina Syokau
Wasanii wa injili Ringtone na Justina Syokau
Image: Instagram//Ringtone//JustinaSyokau2020

Justina Syokau, mwanamuziki wa injili mwenye utata sasa amekanusha kuwa alikuwa anamtamani msanii anayejiita mwenyekiti wa miziki ya injili Kenya, Ringtone Apoko.

 Kulingana na Justina, aliposema kuwa alikuwa anamtamani kimapenzi Ringtone, hakuwa na maana kuwa alikuwa anamtaka yeye bali alikuwa anataka maisha ya Runda na pesa za msanii huyo.

Ikumbukwe kuwa Ringtone kwa muda mrefu amekuwa akijipiga kifua kuwa ndiye msanii tajiri zaidi nchini Kenya akisema anamiliki magari ya kifahari pamoja na jumba la kifahari katika mtaa wa matajiri wa Runda.

Justina alisema kuwa alimsikia Ringtone akisema ana upweke ndio maana akasema alikuwa anamtaka lakini uhalisia ni kwamba alikuwa anatamani kuishi Runda chini ya paa la Ringtone wala si mapenzi.

“Mwenyekiti wa Gospel alisema ako upweke Runda, mimi nikasema sijafika Runda, mimi kusema kuwa nilikuwa namtamani kimapenzi Ringtone haikuwa na maana kuwa ni yeye, nilikuwa natamani Runda, na pesa. Si Ringtone kwa sababu mimi sina haja na yeye bali nilikuwa na haja na maisha ya Runda na pesa. Simhitaji Ringtone, sema tu nimechoka kulipa kodi ya kila mwezi kwa nyumba,” Syokau alisema.

Msanii huyo alisema kwa vile Ringtone alimkwepa, bado maombi yake kwa Mungu yako pale kuwa anataka mwaname tajiri mwaka 2023.

“Ninaomba Mungu anipe tajiri 2023, mwanaume wa kuangaliwa, mzuri ambaye ameenda gym mwili umenyooka,” Justina alisema.

Alidokeza sababu yake ya kuongeza makalio bandia kuwa wengi walimwambia miaka ya nyuma avae nguo za kumsitiri lakini hakupata mwanaume na ndio maana aliamua kuja upya kwa kuongeza makalio.

Kwa ajabu, alisema tena watu walimshambulia hata zaidi wakisema kuwa hiyo si njia ya kumtukuza Mungu.

Ikumbukwe katika mahojiano na mtangazaji mmoja mwaka jana, alidokeza kuwa alikuwa analilia ngoa makalio ya mwanasosholaiti Vera Sidika huku akiapa kuwa angetafuta milioni 3 kwa ajili ya upasuaji wa kuongeza makalio.

Katika mahojiano hayo, Syokau alisema kuwa kuongeza kwake makalio kulikuwa ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu tu wala si kufukuza kiki kwa mambo ya kidunia.