H-Baba adokeza kusaini mkataba WCB Wasafi na kuziba pengo lililoachwa na Rayvanny

Tangu Rayvanny aondoke WCB, lebo hiyo haijapata msanii mwingine wa kuziba pengo lake.

Muhtasari

• Kando na kusaini mkataba, pia msanii huyo alidokeza kuwa anafanya collabo na Diamond mwaka huu.

• Alisema Collabo yake na Mond inakaribia kukamilika kwani mpaka sasa asilimia 97 ya ngoma hiyo iko tayari.

H-Baba adokeza kuchukua nafasi ya Rayvanny WCB
H-Baba adokeza kuchukua nafasi ya Rayvanny WCB
Image: Instagram

Msanii mkongwe wa Bongo Fleva H Baba amefichua kuwa mwaka 2023 ataachia wimbo wake wa kwanza kabisa akimshirikisha Diamond Platnumz ambaye ni bosi wake wa sasa.

Msanii huyo mwenye majigambo si haba alidokeza kwamba wimbo huo ambao ni collabo tayari umeshakamilika kwa asilimia 97 tu swali kubwa ni kuhusu siku rasmi ya kudondosha kitu ambacho alikitaja kama dude la kuteka mawimbi ya miji na vijiji.

Tegemea wimbo mpyaa 2023 H Baba na @diamondplatnumz Umekamilika Asilimia 97 tuombeane DUA,” msanii huyo alisema.

Pia aliwarushia vijembe wabaya wake akisema kuwa anajua fika wengi wao hawafurahi kumuona akiwa pamoja na Diamond ila akawataka wazoee kwani mwaka huu watamuona pamoja na Diamond katika sehemu nyingi tu.

Kando na kutoa wimbo na Diamond Platnumz, msanii huyo alidokeza kuwa yuko karibu kusaini mkataba ili kuziba pengo ambalo msanii Rayvanny aliacha wakati anaondoka katika lebo ya WCB Wasafi.

“Najua kunawatu wanatamani wajinyonge kama nakuona vile hapo unajijua kikubwa @diamondplatnumz kasema H.baba hapa #WCB ndio kwangu ndio nishafika sitoki Ng'oo WCB. Nakaribia kusaini WCB tuombeane Dua ndugu zangu Ongezeni dua,” H-Baba alisema.

Msanii huyo ambaye kabla ya kuwa chawa wa Diamond alikuwa mwandani wa Harmonize, amekuwa kwa mara nyingi akimshambulia rafiki huyo wake wa zamani kwa kusema kuwa ni bahili ambaye hana uwezo wa kutoa pesa kama ambavyo Diamond anafanya kwa watu wanaomzunguka.

Taarifa zake kusaini mkataba kama msanii WCB hazijachukuliwa kwa uzito kutokana na mzaha wake na wengi wanahisi kuwa kauli hiyo ni kama kumnywesha tu machungu Harmonize.

Kwa sasa, H-Baba ni balozi wa mauzo katika kampuni ya bahati nasibu ya Wasafi Bet inayomilikiwa na Diamond Platnumz na pia anajiongeza kama chawa wa msanii huyo.