Lilian Ng'ang'a ataja funzo kuu kutoka kwa mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ, Chiloba

Ng'ang'a alisema hisia za kimapenzi ndizo hisia kuu zaidi duniani.

Muhtasari

• Awali, wanajamii ya LGBTQ walikuwa wanaomboleza kuwa mwenzao aliuawa kutokana na chuki dhidi ya jamii hiyo.

• Baadae ilibainika kuwa huenda aliuawa na mpenzi wake ambaye ndiye mshukiwa mkuu aliyeko kizuizini.

Ng'ang'a azungumzia fundisho kutoka kwa mauaji ya Chiloba
Ng'ang'a azungumzia fundisho kutoka kwa mauaji ya Chiloba
Image: Instagram

Huku Wakenya na walimwengu kwa jumla wakiwa wamezama katika gumzo kuu la mauaji ya mwanaharakti wa jamii ya kutetea mapenzi ya jinsia moja, LGBTQ, Edwin Kiprotich Kiprop almaarufu Chiloba, watu mbali mbali wameendelea kutoa hisia zao kuhusu sakata hilo.

Kwa kawaida, ilitarajiwa kuwa watu kutoka jamii ya LGBTQ ndio wangelivalia njuga suala hilo lakini sasa baada ya kugundulika kuwa hakuuawa kutokana na chuki dhidi ya wanajamii hao bali kutokana na mzozo wa kimapenzi na mpenzi wake wa kiume, tukio hilo limechukua mkondo tofauti ambao umeona hata wale wasiojihusisha na masuala ya LGBTQ wakizungumza kwa hisia.

Mauaji ya Chiloba ambaye alipatikana ameuawa na mwili wake kukunjwa ndani ya sanduku la chuma yamegeuka sasa kuwa ni mauaji ya kikatili tu katika mzozo wa kimapenzi na si mauaji kutokana na mrengo wake wa kupigania LGBTQ.

Hilo limekuwa fundisho kubwa katika Wakenya wengi na aliyekuwa mke wa gavana wa kwanza wa Machakos, Alfred Mutua, Lilian Ng’ang’a amekuwa wa hivi punde kulizungumzia hilo.

Kulingana na Ng’ang’a ambaye ni mama wa mtoto mmoja na mke wa mwanamuziki Juliani, fundisho kubwa kutoka kwa mauaji yake ni kwamba kila mtu ana hisia za kimapenzi, haijalishi unapenda mtu wa jinsia tofauti au unapenda mtu wa jinsia kama yako – hisia za kimapenzi ni zile zile.

Ng’ang’a alisema kuwa amejifunza hisia hizo za kimapenzi zikiendekezwa na wivu katika uhusiano basi huenda zitasababisha madhara makubwa zaidi ambayo hata shetani mwenyewe atachukua likizo kuyatathmini.

Pia alisema haijalishi ni huba la aina gani, hisia hizo zinaweza sababisha mtu kuwa mzuri au mbaya kulingana na jinsi atakavyokabili hali yenyewe.

“Kutoka kwa kesi ya mauaji ya Chiloba pamoja na visa vingine vya mauaji ambavyo tunasikia kila siku, hatuwezi kata kuwa; mapenzi ndio hisia kuu zaidi katika dunia. Na hisia hizo zinaweza tufanya tuwe bora au wabaya zaidi,” Lilian Ng’ang’a alisema.

Wewe umejifunza nini kutokana na kesi hiyo?