Manara arudi kwa mke wa kwanza na kuomba msamaha baada ya kuachwa na mke wa 2

"Nakuomba nisamehe tena sisi binadamu hukosea ni maumbile yetu mke wangu" - Manara.

Muhtasari

• Msamaha huo kwa mke wa kwanza unakuja siku chache baada ya habari kuzagaa kuwa ameachwa na mke wa pili.

Haji Manara na wake zake wawili
Haji Manara na wake zake wawili
Image: Instagram

Mwaka ndio kwanza ni mpya kabisa lakini tayari chini ya siku kumi mambo mengi katika Sanaa ya burudani ukanda wa Afrika Mashariki yametokea.

Taarifa mpya zinadai kuwa huenda msemaji wa timu ya Yanga nchini Tanzania Haji Manara ametemwa na mke wake wa pili, miezi kadhaa tu baada ya kujionesha na kujipiga kifua jinsi ana ustadi katika kuwahendo na kuwamudu wanawake wawili.

Kwa wiki kadhaa, Manara ambaye alikuwa akionekana na wake zake wawili kila sehemu alianza kuonekana na mke wa kwanza tu huku wengi wakiibua maswali kuhusu uwepo wa mke wa pili kwa jina Rushaynah.

Lakini Manara mwenyewe kama alivyo sungura, aliwaaminisha wadadisi hao kuwa mkewe Rushaynah alikuwa mgonjwa na ndio maana hakuwa anaonekana naye kama awali.

Mashaka yaliendelea kutanda miongoni mwa wale waliokuwa wakililia ngoa uhusiano wake na wanawake wake ila sasa ni kama bomba limejaa pomoni mpaka kushona, na hakuna tena nafasi ya uongo kujificha maana ukweli umeelea.

Haji Manara na mkewe wa pili, Rushaynah wote kwenye mtandao wa Instagram hawafuatani tena kama awli, yaani kila mmoja ameamua kujishughulisha na hamsini zake.

Kitendo hicho kinadhibitisha kwa asilimia kubwa kuwa huenda Rushaynah amejiondoa katika ndoa hiyo ya utatu na katika blogu moja ambayo ilipakia video ya zamani wakichezeana na Manara, Rushaynah mwenyewe alifika pale na kutaka video ile iondolewe mara moja kwani kwa kuiona tu anachefuka.

Blogu ya bongotrending inachapisha video hiyo na kuinukuu, “Manara na pisi lake.”

Rushaynah kwa haraka mno alifika pale na kutoa tamko lililowaacha wengi katika maswali mengi akisema, “wewe koma, hebu futa.”

Kama hilo bado halijapoa, usiku wa kuamkia Jumanne, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram aliachia ujumbe mrefu akimuomba msamaha mke wake wa kwanza Rubi kwa kumletea mke wa pili huku pia akimtakia kila la kheri katika safari yake ya ujauzito na kujifungua salama.

Manara alisema pamoja na mke wake wa kwanza, wamedumu kwenye ndoa kwa miaka 7.