Njaa ya Januari inafanya watu kufananisha zulia la nyumba yangu na Omena - Wahu

Ni kweli ugumu wa Januari unafanya watu kuwaza vyakula wanapoona vitu vyenye mshabihiano navyo?

Muhtasari

• Kwa umbali, Zulia hilo linaonekana kama omena wengi ambao wametapakazwa sakafuni.

Wahu asema zulia lake si omena
Wahu asema zulia lake si omena
Image: Instagram

Mwanamuziki Wahu Kagwi amesema kuwa baada ya kupakia video akionesha mume wake Nameless pamoja na binti yake wa pili Nyakio wakiwa wanamlea mtoto wake mchanga Shiru ndani ya nyumba yao, watu walianza kuchanganya zulia la nyumba hiyo ya kifahari na samaki aina ya omena.

Katika video hiyo aliyopakia kwenye Instastories zake, Nameless na Nyakio walionekana wametebwereka kwenye sakafu yenye zulia la kahawia iliyofifia na rangi mikunyato ya zulia hilo pamoja na makopakopa yalikuwa na taswira kama ya Omena ambao wamemwagwa sakafuni kukauka.

Wahu alizua mzaha kuwa watu wengi walioona video hiyo waliianza kumwandikia jumbe na meseji wakitaka kujua ni kwa nini familia yake inakali Omena – chakula, wakati huu msimu wa Januari wengi wanauhusisha na ukame pamoja na njaa.

“Baadhi ya watu huku nje wameanza kuchanganya zulia langu na Omena, enyewe ni Januari,” Wahu aliandika kwenye video moja huku pia akifuatisha na picha ya watu ambao walikuwa wanasema walifikiri ni Omena wamekaliwa.

"Huyo ni mimi kabisa, niliona Omena wengi ajabu," Joyz Cheps alisema.

"Kusema kweli tu tuache utani, lakini zulia linakaa kama liko na Omena wengi," mwingine alisema.

Wahu alikuwa anaonesha jinsi mpya ya kurahisisha malezi kwa mwanawe Shiru ambaye sasa hakuwa analelewa mikononi bali ndani ya kiti chake cha starehe kwa lugha ya kimombo "Baby Rocker"