Mwanaume amevalia kitenge ni mume wa mtu - Samidoh ashauri

Msanii huyo alisema kuwa hakuna mwanamume anayevalia nguo hiyo kwa kupenda bali kushrutishwa na mwanamke.

Muhtasari

• Wengine walimwambia angevaa kitenge ili Nyamu asimkaribie akijua kuwa ni mume wa mtu.

Samidoh atoa ushauri kuhusu wanaume wa vitenge
Samidoh atoa ushauri kuhusu wanaume wa vitenge
Image: Instagram

Afisa wa polisi ambaye pia ni mwanamuziki wa Mugithi, Samwel Muchoki almaarufu Samidoh ametoa ushauri kwa wanadada ambao wanatafuta wanaume ambao wako singo.

Samidoh amewataka wanawake hao katika kuhakiisha kuwa hawaangukii mwanamume ambaye tayari ana mwanamke wake, ishara ya kwanza ni kuangali kama anavalia nguo aina ya kitenge.

Samidoh alisema kuwa ukimuona mwanamume yeyote amevalia nguo hiyo basi jua moja kwa moja bila maswali mengi kuwa huyo ni mume wa mtu. Samidoh alitetea ushauri huo wake kwa kusema kuwa uzoefu alio nao katika mapenzi, hakuna mwanamume anapenda kuvaa nguo kama hiyo bali wengi ambao huzivaa ni kushrutishwa kutoka kwa wanawake zao.

“Mwanaume aliyevaa kitenge ni wa mtu 😊, hakuna mwanaume anayevaa hizo nguo kwa kupenda,” Samidoh alitoa ushauri kwa wanadada.

Katika kauli kama hizi zenye ukakasi uliokolezwa munyu, bila shaka hapakosi wambea. Baadhi walimshauri kuwa angejua huu ushauri mapema pengine asingejipata kwa mtego wa seneta Karen Nyamu mpaka kuzaa watoto wawili naye hali ya kuwa bado ana mke wa kwanza.

Walimwambia kuwa angevaa kitenge mapema kama ishara ya Nyamu kuona ni mume wa mtu na hivyo kumkwepa.

Sakata la Nyamu na Samidoh limekuwa likizungumziwa mitandaoni kwa mwaka wa tatu sasa tangu liwekwe bayana alipoomba mkewe Edday Nderitu msamaha wa hadharani kuwa alikosea kuenda kwa Nyamu na kuwa alijuta – jambo ambao hata hivyo alionekana kulirudia tena na tena, kwani muonja asali siku zote hawezi onja mara moja.

Mwishoni mwa mwaka jana baada ya sekeseke za Dubai baina yake na wanawake wake wawili, Nyamu alitangaza kujiondoa katika uhusiano huo na kusema ndio mara ya mwisho kwa watu kumuona na mwanamuziki huyo.

Hata hivyo, baadhi wanahisi yale yalikuwa ni maneno tu na kadri siku zinasonga, wataonekana tena pamoja wakioneshana mahaba yao kama kawaida.

Ikumbukwe Nyamu na Samidoh wana watoto wawili ndani ya miaka 3 ya uhusiano wao.