Stephen Letoo: Niliishi Kawangware kwa kula ugali na nyanya zilizooza za senti 50

Letoo alisema maisha yake akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu kwa miaka 4 yalikuwa na shida siku zote kwa kipindi hicho.

Muhtasari

• Mwanahabari huyo maarufu alifunguka kuwa katika miaka 4 ya chuo kikuu, mfuko wake ulikuwa fukara muda wote.

Mwanahabari Stephen Letoo.
Mwanahabari Stephen Letoo.
Image: Facebook

Mwanahabari maarufu wa runinga ya Citizen Stephen Letoo amefunguka kuhusu maisha yake ya chuo kikuu kwa miaka minne jinsi yalivyokuwa ya karaha na uhayawinde mkali jijini Nairobi.

Akizungumza katika kipindi cha Behind the Mic na na mwanahabari wa kituo kimoja cha shirika la Royal Media, Letoo alisema kuwa alikuwa anaishi katika mtaa duni wa Kawangware ambapo maisha yake kucha kutwa yalikuwa na nembo ya shida katika panda la uso wake.

Letoo alisema kuwa alifika Nairobi akiwa mtu duni asiye na ujuaji wowote wa jiji huku akiwa na matumaini makubwa ya kutusua kimasomo katika chuo kikuu pasi na kutegemea mzazi kwa matunzo.

Mwanahabari huyo alisema kuwa enzi hizo akiwa mtaa wa Kawangware, alilazimika kununua nyanya zilizooza kwa senti 50 ili kuzitumia kama mboga kwa ugali wake ambao alikuwa anaupata kwa nadra sana.

“Maisha yalikuwa magumu kweli bila chanzo cha mapato na tegemeo la wazazi. Nilikuwa sina pesa wakati wote. Nilikaa Kawangware nakumbuka nilinunua nyanya mbovu kwa senti 50 na nilikuwa nakula na ugali na kumaliza siku. Nilikuwa chuoni kwa miaka minne, ndivyo hali ilivyokuwa mbaya kwangu wakati huo,” Letoo alimwambia Mwangi Cynthia.

Ripota huyo maarufu wa masuala ya kisiasa alisema kuwa alipata msukumo wa kusomea uanahabari kutokana na babake kumiliki runinga ndogo mbovu enzi hizo ambayo wanakijiji wengi walikuwa wanafurika nyumbani kwao kwa ajili ya kufuatilia habari.

Baada ya kutusua kwa tasnia ya uanahabari, Letoo anajivunia kuwa mmoja wa wanahabari maarufu ambao mpaka rais Ruto alipata kuwatumia salamu siku ya kuapishwa kwake kutokana na kasi yake ya kufuatilia na kupeperusha habari za kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka jana.

"Nimezunguka ulimwengu, nimekutana na watu warembo na wa ajabu, nimekuwa na uzoefu wa kunyenyekea na wakati wa kampeni za urais zilizomalizika hivi karibuni 2022 nilikuwa mstari wa mbele kuripoti matukio kama yalivyotokea, ambayo yalikuwa ya kusisimua sana, kasi na adrenaline ya kampeni ilikuwa uzoefu wa kujifunza,” alisema.