Mwaka huu mpango wa kando afure tumbo, apate mimba tasa! - Pastor Ezekiel

Mchungaji huyo aliwakemea michepuko wanaofaidi kutokana na mapato ya wanaume walioko kwenye ndoa huku akiwatamkia laana kali.

Muhtasari

• Mchungaji Odero alisema kuwa kuna mipango ya kando wanaishi vizuri kuliko wake halali wa ndoa. 

• Alisema mwaka huu watakoma kwani laana ya Mungu itawashukia ambapo watafura tumbo bila kitu ndani.

mchungaji Ezekiel Odero
mchungaji Ezekiel Odero
Image: Facebook

Mchungaji mwenye utata, Ezekiel Odero ametamka laana kwa wanawake michepuko ambao wanasherehekea mishahara na mapato ya wanaume walio na ndoa huku wanawake halali katika ndoa hiyo wakisaga meno.

Katika video moja ambayo ilionekana Tiktok Odero akihubiri katika kanisa lake lililopo Mavueni kaunti ya Kilifi, alisema kuwa si haki hata kidogo kwa michepuko kufurahia matunda ambayo mke halali anafaa kufurahia kwenye ndoa.

Mchungaji huyo alisema kuna michepuko ambao wanaishi maisha ya starehe kutokana na pesa na mali ya mwanaume ambaye mke wake ni mtu ayayeishi maisha ya uhayawinde mkubwa.

Kila moja aende akule mshahara wa bwanake. Wewe unajua kuna watu wanaendesha magari yaliyonunuliwa na mabwana za wengine? Watu wako na maghorofa ambayo wamejengwa na mabwana za wengine. Watu wako na mashamba! Mtu anapigwa kwa nyumba na mpango wa kando ananuniliwa nyumba,” mchungaji huyo alihubiri kwa hasira.

Alitamka laana kuwa mwaka huu mwanamke yeyote ambaye ataendelea kumchuna mume wa wenyewe atapata pigo la kufura tumbo ambalo litakuwa kama ujauzito lakini hakutakuwa na ujauzito.

“Mpango wa kando ambaye ataenda kula pesa ya mume wa watu na afure tumbo, apate mimba tasa isiyo na mtoto,” Odero alitamka laana hiyo huku akiwaamrisha waumini wake kila mmoja kugeukia jirani yake na kumtaka kukasirika ili laana hiyo inate.

Mchungaji huyo amejulikana kutokana  na mahubiri yake yenye utata ambayo yamekumbatiwa pakubwa na wananchi wengi, asilimia kubwa ikiwa ni kina mama.

Mwishoni mwa mwaka jana, Odero aiwafokea watu wazima wanaosherehekea Krismasi huku akisema kuwa sherehe hizo zinafaa kuwa za watoto na mtu mzima na akili zake hafai kusherehekea.