Mwaka wa kupanuliwa: Justina Syokau apewa V8 kama zawadi ya siku yake ya kuzaliwa

Msanii huyo anaendelea kutamba na wimbo wa kupanuliwa mipaka ya mafanikio na baraka katika mwaka 2023.

Muhtasari

• “Nilipokea zawadi ya kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa, zawadi yenye thamani ya mamilioni ya pesa" - Syokau.

Syokau apewa zawadi ya V8
Syokau apewa zawadi ya V8
Image: Instagram

Mwishoni mwa wiki jana, mwanamuziki wa injili Justina Syokau alikuwa anaseheherekea siku yake ya kuzaliwa.

Msanii huyo ambaye anazidi kutamba kwa wimbo wa mwaka wa 2023 akisema ni wake wa kupanuliwa mipaka ya mafanikio, aliwataka watu na mashabiki wake wenye roho safi kumpa zawadi kwa wingi ili kutia nakshi siku hiyo.

Sasa Justina amefichua kuwa katika zawadi nyingi alizopewa, moja yao ilikuwa ni gari la kifahari aina ya Toyota Landruiser V8.

Ili kuwatoa wasiwasi wale waliokuwa wakisema ni uongo, msanii huyo alipakia rundo la picha na video akiwa kando na gari hilo la rangi nyeupe likiwa limepambwa kwa maua na minara maridadi ambalo lilipokezwa kwake kama zawadi ya kusherehekea kuongeza mwaka mwingine.

“Nilipokea zawadi ya kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa, zawadi yenye thamani ya mamilioni ya pesa. Ninashukuru sana,” Justina aliandika pasi na kufichua mtu au kampuni gani iliyojitoa kwa kiasi hicho kikubwa.

Katika moja ya video amabzo alichapisha Instagram, Syokau alionekana akiwa anatembea huku ameandamana na wanaume ambao wanakisiwa kuwa ndio walimkabidhi hiyo zawadi ambayo hakuwa anatarajia.

Wanaume hao wanaongozanqa naye huku mmoja akiwa amemfumba macho kwa kiganja chake na walipomfikisha kwenye gari hilo, Justina aliliona na kupiga magoti chini kwa kusujudu huku akiwa kama anatokwa na machozi ya furaha.

Licha ya vidhibitisho hivyo vyote kuwa gari ni zawadi yake halali, wengi bado walisema hawawezi kumuamini mpaka pale atakapowaonesha hati za kumiliki gari hilo, huku wakimtuhumu kwa kutumia muda mwingi katika kutafuta kiki ili kupata kuzungumziwa mitandaoni na kwenye mablogu.

Ikumbukwe mwishoni mwa mwaka jana kabla ya kutoa wimbo wa 2023, Syokau alidanganya kuwa amefanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio, jambo ambao lilikuja kugundulika kuwa ni uongo.

Kama kweli hilo gari ni zawadi yake, basi bila shaka yoyote huenda maombi yake katika mwaka huu yameanza kupanuliwa na atatarajia mengi.