"Nilizaliwa baada ya miezi 11", - Bonnie Musambi afichua akisherehekea siku yake ya kuzaliwa

Mtangazaji huyo wa muda mrefu alisema baba yake alimpa jina "Mutisya" kumaanisha mtu wa kuchelewesha hedhi ya kuzaliwa.

Muhtasari

β€’ Alisema kuwa baba yake baada ya kumpa jina hilo alimtabiria kuwa atakuwa mtu wa kupata mafanikio makubwa maishani.

Mtangazaji Bonnie Musambi
Mtangazaji Bonnie Musambi
Image: Facebok

Aliyekuwa mtangazaji Bonnie Musambi Jumatatu January 16 alikuwa anasherehekea kuzaliwa kwake ambapo mkewe alimtungia ujumbe maalum wa kumsherehekea.

Musambi kwa upande wake pia aliachia ujumbe mrefu kweye ukurasa wake wa Facebook akisimulia jinsi kuzaliwa kwake kulikuwa si kwa kawaida.

Musambi pia alitumia fursa hiyo kusimulia maana ya jina lake la pili la Mutisya lina maana gani.

Alisema kuwa alizaliwa baada ya miezi 11, kinyume na miezi 9 ya kawaida ambayo ndio inajulikana, jambo ambalo lilipelekea baba yake kumpa jina hilo ambalo kwa jamii ya Akamba lina maana ya mtu aliyechelewesha ujauzito.

β€œHalo Watu Wote πŸ‘‹, Kula, kunywa na kufurahi kwa sababu ni siku yangu ya kuzaliwa!😊😊😊 Kwa namna fulani, unajua kuzaliwa kwangu kulikuwa na utata kidogo? Nilizaliwa Ijumaa tarehe 16 Januari, 9.30pm, BAADA YA MIEZI KUMI NA MOJA (Siyo tisa). Baba yangu aliniita MUTISYA, kwa kuchelewesha hedhi ya kawaida ya kuzaliwa. Kisha akatabiri kwamba siku zote nitafanikiwa mambo makubwa katika ulimwengu huu (Amina kwa hilo). Ninampa Mungu Utukufu wote kwa kunitunza muda wote huu; kwa dhati siichukulii poa. Pia ninaishukuru familia yangu kwa upendo na utunzaji wa ajabu,” Musambi alisimulia.

Musambi ambaye kwa sasa ni mjasiriamali katika tasnia ya habari na mawasiliano anaendesha kituo chake cha redio kinachopeperusha matangazo kwa lugha ya Akamba.

Alipata umaarufu mwingi wakati anafanya katika idhaa ya kitaifa ya KBC ambapo alihudumu kwa miaka 14 kabla ya kuachia kazi hiyo.

Baada ya kuondoka katika idhaa ya kitaifa, alienda kuwania ubunge wa Kitui ya kati ila hakufanikiwa kupata wadhifa huo.