"Siachi pombe!" Karen Nyamu abadili msimamo wake

“Mbona niache,” Nyamu alijibu shabiki aliyetaka kujua kama ukweli aliacha kutumia pombe.

Muhtasari

• Mwaka jana, Nyamu aliapa kuwa ameacha kunywa pombe kufuatia sakata la Dubai ambapo alisema ulevi ndio ulimtuma kuleta aibu katika shoo ya Samidoh.

Nyamu asema haachi pombe
Nyamu asema haachi pombe
Image: Facebook

Seneta mteule Karen Nyamu amedokeza kuwa hawezi acha kunywa pombe licha ya awali kuapa kuwa ameacha kutumia vilevi vyovyote kufuatia sakata la aibu lililotokea Dubai likimhusisha na kuburuzana na Edday Ndritu – mke wa kwanza wa msanii Samidoh ambaye walikuwa wanapigania.

Nyamu aliweka chapisho kwenye Facebook yake akinukuu kifungu cha Biblia kuwataka watu wasiwe watumwa. Hapo ndipo shabiki yake mmoja ambaye pia ni mwanasiasa alimtupia swali la kutaka kujua iwapo aliacha kunywa pombe.

Nyamu alijibu kuwa alijaribu kuacha lakini akatathmini sababu za kumfanya aache kunywa pombe wala hakupata.

“Tulinunuliwa kwa bei; Msiwe watumwa wa Wanadamu. - 1 Wakorintho 7:23.Nawatakia kila la kheri baraka za Mungu,” Seneta Nyamu aliandika.

“Natumai uliacha pombe,” Douglas Maraga alimuuliza.

“Mbona niache,” Nyamu alijibu.

Mwishoni mwa mwaka jana, baada ya mchezo wa kuigiza huko Dubai, mwanasheria huyo alienda kwenye kikao cha moja kwa moja akielezea matendo yake.

Nyamu, ambaye alikuwa kitovu cha ugomvi na babake mtoto, mwimbaji maarufu wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alikosoa pombe hiyo kwa tabia yake mbaya.

Nyamu alienda kwenye meza ambayo mwimbaji Mugithi alikuwa ameketi na mkewe na kukaa kwa nguvu kwenye mapaja yake. Katika klipu nyingine, anaonekana akiruka jukwaani na kucheza huku babake mtoto akitumbuiza.

Kitendo hicho cha kuzua rabsha katika shoo ya Samidoh kilimkaribishia matatizo kupelekea kuitwa mbele ya kamati ya nidhamu na adhabu ya chama tawala cha UDA ambacho kilimteua katika bunge la seneti.

Baadhi ya mashabiki wake wanahisi kwamba si tu ahadi ya kuacha pombe amekiuka bali pia hivi karibuni huenda atasaliti maneno yake kuwa hatowahi rudiana na Samidoh tena na huenda wakaanza kuonekana pamoja.