Fahamu kwa nini Nandy atawasaini wasanii wa kike tu kwenye lebo yake mpya

"Kama tunavo ona sanaa ya watoto wa kike ni chache sana na uthubutu umekuwa ni mdogo," - Nandy.

Muhtasari

• Nandy alisema tayari amemsaini msanii mmoja wa kike ambaye ataachia wimbo wake Alhamisi hii.

Nandy afungua lebo yake mpya
Nandy afungua lebo yake mpya
Image: Instagram

Malkia wa muziki wa Bongo Fleva Nandy ametangaza kufungua lebo yake ya muziki ambayo itaanza kufanya kazi mara moja.

Msanii huyo alizindua lebo hiyo kwa jina African Princess siku ya Jumatatu alasiri na kuweka wazi kuwa haitakuwa lebo ya kawaida.

Alisema itakuwa ni lebo ya kipekee kwa ajili ya wasanii wa kike tu ambao alisema ndio walimpa msukumo wa kuwainua na kuwakimu katika Sanaa ya muziki ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikitawaliwa na wanaume.

Nandy alisema kuwa tayari lebo hiyo imemsaini msanii mmoja ambaye Alhamisi hii ataachia ngoma yake ya kwanza.

“Ninayo furaha kubwa kuileta kwenu Rasmi THE AFRICAN PRINCESS LABEL…! 2023 lebo ambayo itahusisha wanawake tu! Kama tunavo ona sanaa ya watoto wa kike ni chache sana na uthubutu umekuwa ni mdogo kwa hiyo tuna imani na kuomba lebo ya African princess itaongeza wingi wa vipaji vya watoto wa kike waliopo mtaaani wenye ndoto kubwa ya kuwa wanamziki!!” Nandy alisema.

Msanii huyo mwenye mafanikio makubwa kimuziki alisema kuwa lebo hiyo haitaangazia vipaji vya watoto wa kike tu kutoka Tanzania bali itatanua mbawa zake kote Afrika kujaribu kuwakimu na kuwainua wasanii wa kike ambao mara nyingi huombwa rushwa ya ngono ili kupewa nafasi ya kurekodi muziki katika lebo nyingi zinazoongizwa na wanaume.

Aliwataka washikadau wote katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kumpa shavu na kufanikisha ndoto hiyo.

“Lakini pia hii labo SIO ya wa Tanzania tu! Ni labo ya AFRIKA. Kwa hiyo tutarajie kuona vipaji mbali mbali kutoka nchi mbali mbali. Ndio maana inaitwa AFRICAN PRINCESS LABEL. Shukrani za dhati kwa watu wote walio pokea hili huu ni mwanzo kaa karibu na Mtandao wako maaana hivi karibuni tutamzindua msanii wetu wa kwanza!!!!” alisema.