"Nilikuwa na msongo wa mawazo" Kanambo Dede awashukuru Nana Owiti, King Kaka kwa kumwokoa

Rapa huyo amewashukuru wanandoa hao kwa kumuokoa wakati ambapo alikuwa katika hali mbaya.

Muhtasari

•Rapa huyo kijana alifichua kuwa alikuwa amezama kwenye msongo wa mawazo kabla ya kukutana na Bi Owiti.

•Msanii huyo alidokeza kuwa mambo yalibadilika baada ya Bi Owiti kumwalika washiriki chakula cha mchana pamoja.

King Kaka, Kanambo Dede na Nana Owiti
Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwimbaji Quincher Kanambo amemshukuru mtangazaji Nana Owiti na mume wake mwimbaji  King Kaka kwa kumuokoa wakati ambapo alikuwa katika hali mbaya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, rapa huyo kijana alifichua kuwa alikuwa amezama kwenye msongo wa mawazo kabla ya kukutana na Bi Owiti.

Kanambo alisema kuwa kulea mtoto mdogo peke yake katika umri wake mdogo haikuwa rahisi kwake hata kidogo.

"Nilikumbwa na msongo wa mawazo sana. Na nililelewa na mama single kwa hivyo najua jinsi ambavyo inauma. Nilimhurumia mwanangu na nilijilaumu kwa kufanya uamuzi wa kijinga sana," aliandika.

Msanii huyo alidokeza kuwa mambo yalibadilika baada ya Bi Owiti kumwalika washiriki chakula cha mchana pamoja.

"Nilikuwa namtazama kwenye Switch TV sikuwahi kufikiria kuwa angeweza kuleta athari kubwa sana katika maisha yangu ya ujana," Alisema.

Kufuatia hayo, Kanambo ametoa shukrani za dhati kwa mtangazaji huyo na mumewe kwa mchango wao mkubwa katika maisha yake.

Katika majibu yake, Nana alijivunia kile alichomfanyia mwanadada huyo na kumtaka awatie moyo wanawake wengine.

"Wow, nafurahi kuwa na ushawishi chanya, si kwa wewe tu bali wasichana wengi katika shida yako. Pitisha kijiti. Nakupenda ❤️ 🙌," Nana alijibu.

Mwezi Julai mwaka jana, Kanambo Dede alirejea katika shule ya upili kwa ajili ya kukamilisha masomo yake kwa usaidizi wa wanandoa hao.

Kanambo ambaye alijizolea umaarufu mkubwa mapema mwaka jana alijiunga na shule mpya ili kuendeleza masomo kutoka alikoachia.

King Kaka ndiye aliyefichua habari hizo na kuweka wazi  kuwa hayo ni matakwa ya mama huyo wa mtoto mmoja.

"Alitamani, ilifanyika leo. Kanambo Dede amerudi shuleni," King Kaka alitangaza mnamo Julai kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake, mkewe Nana Owiti na msanii huyo wake ambaye alikuwa amevalia sare ya shule.

Nana Owiti alisema hatua ya Kanambo kurudi shuleni ilimsisimua sana nusura abubujikwe na machozi.

Alifichua kuwa yeye na mumewe walienda kumtafutia Kanambo shule nzuri baada ya kuwaambia kuwa anataka kukamilisha masomo yake.

"Moja ya matukio makubwa zaidi yalifanyika leo, @quinchermkanambo alitaka nafasi ya pili shuleni. Mara akauliza, nilimuuliza kama yuko tayari kukata dreadi zake ili tu nione mahali kichwa chake kilipo na akajibu mara moja kwa uthibitisho. Tumekuwa tukimtafutia shule nzuri yeye binafsi ( King Kaka na mimi) Kwa ufupi, amejiunga na shule leo na nilihisi kulia 😢, " Bi Owiti alisema kupitia Instagram.

Katika ujumbe wake mtangazaji huyo pia  aliwasihi Wakenya kuziunga mkono ndoto za Kanambo kwa njia yoyote ile.