Victor Bwire wa MCK ajitenga na Victor Bwire, mshukiwa wa ugaidi na Al Shabaab

Alisema kuwa yeye ni Victor Lupia Bwire na hana uhusiano wowote na Victor Odende Bwire aliyefikishwa mahakamani kwa kushirikiana na Al Shabaab.

Muhtasari

• Mshukiwa huyo alishtakiwa kwa kutoa taarifa za Kijasusi kwa kundi la Al Shabaab kuhusu uwezekano wa kuvamia jumba la KICC.

Victor Bwire, Mkurugenzi wa mafunzo katika baraza la MCK
Victor Bwire, Mkurugenzi wa mafunzo katika baraza la MCK
Image: Facebok

Mkurugenzi wa Mafunzo na Maendeleo ya Vyombo vya Habari katika Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya - MCK, Victor Bwire amejitenga na madai ambayo yamekuwa yakisambazwa mitandaoni akifananishwa na mwanamume mmoja aliyeshtakiwa mahakamani kwa kutoa taarifa za kijasusi kuwezesha Al Shabaab kushambulia Jumba la KICC.

Jumatatu, mahakama ya Milimani jijini Nairobi ilimsomea mwanamume mmoja kwa jina Victor Odende Bwire, mashtaka ya kutoa taarifa za kijasusi kwa wanamgambo wa Al Shabaab ambao walikuwa wanapanga kulipua KICC jijini Nairobi mwaka 2019.

Baada ya majina ya mshukiwa huyo kufanana na yale ya mkurugenzi wa mafunzo katika baraza la MCK, Bwire aliingia kwenye akaunti yake ya Facebook na kujitakasa kwa haraka akisema kuwa si yeye bali ni mshabihiano tu wa majina.

Baada ya kutoa tamko lake, tofauti ilionekana kuwa jina la kati tu.

Wadau mimi ni Victor Lupia Bwire OGW. Ndio mimi hapa....naendelea kuhudumia wanachama... watu wasiwachanganye,” Bwire wa MCK alisema na akiwa amepakia picha yake.

Awali Jumatatu asubuhi, Hakimu Mkuu wa Milimani Bernard Ochoi alimpata Victor Odende Bwire na hatia ya kosa la kula njama ya kutekeleza shambulizi la kigaidi na atahukumiwa Februari 8, 2023.

Bwire alishtakiwa kwa kukusanya taarifa kwa nia ya kufanya shambulizi la kigaidi kwenye jengo la kihistoria la KICC.

Maelezo ya mashtaka yalisoma kuwa, mnamo Januari 23, 2019, katika mtaa wa Umoja, Nairobi, alinakili pamoja maelezo kuhusu usalama wa KICC na kusambazia washirika wa ugaidi kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii. Alikamatwa Aprili 9, 2019.

Imehaririwa na Davis Ojiambo.