Diamond na Alikiba waombwa kuiga mfano wa Wizkid na Davido kuzika tofauti zao

Wasanii hao wawili kutoka Nigeria kwa muda mrefu wamekuwa wakitupiana vijembe kuhusu nani mbabe na mkali.

Muhtasari

• Mashabiki waliwataka wasanii Alikiba na Diamond kuiga mfano kama huo na kukomaa kwani wamepita kiwango cha kuoneana bifu za kudumaza.

• Pia mashabiki walitoa tamko kali kwa Harmonize na Rayvanny na kukashfu kitendo cha kuvuana nguo kilichotokea mapema wiki hii.

Aliiba na Diamond waambiwa wajifunze kutoka kwa Wizkid na Davido
Aliiba na Diamond waambiwa wajifunze kutoka kwa Wizkid na Davido
Image: Instagram

Baada ya miaka mingi ya vita vya ubabe kati ya wasanii wenye majina makubwa utoka Nigeria, Wizkid na Davido, wawili hao sasa wamepita hapo na hivi karibuni watakuwa kwenye jukwaa moja.

Siku ya Jumatano 18, 2023, Wizkid aliingia kwenye Instagram story yake na kutangaza kwamba kwa kushirikiana na Davido, watafanya ziara ya muziki baada ya ziara ya albamu yake ya tano ya studio ‘More Love, Less Ego (MLLE)’.

“Baada ya ziara yangu ya ‘MLLE (More Love, Less Ego)!! Davido na mimi tutakwenda kwenye ziara! kuokoa sarafu yako! Na sitaki kusikia kitu chochote,” aliandika kwenye Instagram.

Inaarifiwa Davido alitia emoji ya upendo kwenye komenti hiyo kwa ishara kuwa amekubali na mwisho wa bifu lao la muda mrefu umefika.

Habari hii ni ya kushangaza kwa mashabiki, ambao wametarajia ushirikiano kati ya wawili hao kwa muda.

Mashabiki walishangazwa na hilo walipotazama wasanii wanaowapenda wakitumbuiza pamoja jukwaani kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.

Tayari mashabiki wamefurahishwa na ziara ya waimbaji hao wawili wa Nigeria, huku baadhi yao wakiwatia moyo kuachia wimbo mpya kabla ya kuanza kwa ziara hiyo.

Taarifa za wawili hao kufanya ushirikiano kisanaa na kuzika tofauti zao za kibabe zinakuja wiki ambayo katika ukanda wa Afrika Mashariki kumekuwa na sekeseke mitandaoni wasanii Harmonize na Rayvanny wakichafuana vikali.

Mashabiki wa ukanda huu waliwataka wawili hao kuiga mfano wa wenzao kutoka Nigeria na kukoma kufanya vitendo kama hivyo vya kudumisha juhudi zao za muda mrefu.

Pia mashabiki walituma ujumbe kwa Alikiba na Diamond ambao kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa wasanii wasioweza kuonana jicho kwa jicho.

Mashabiki hao ambao walifurika kwenye mitandao ya kijamii walisema kuja pamoja kwa Wizkid na Davido ni ujumbe mkubwa kwao kuwa ni wakati sasa umefika ambapo wote wana mafanikio makubwa kimuziki, kuzika tofauti zao na kushirikiana kuisogeza Sanaa ya muziki wa ukanda huu mbele zaidi.

Walisema kuwa miaka si mingi wawili hao watastaafu katika muziki, na kuwataka kuacha picha nzuri ya kuoneshana upendo na ushirikiano, kwani ndicho kitu ambacho kitalainisha historia yao siku za usoni kwa herufi za dhahabu.