Ntalami: Nitamtangaza mpenzi wangu wakati ukifika na niwe na uhakika 100% ni wangu

"Acha. Hadi mimi mwenyewe nithibitishe uhusiano wangu, acha uvumi.” - Michelle Ntalami alisema.

Muhtasari

• Nina marafiki kadhaa wa kiume na wa kike. Ninaomba watu waache kudhani kuwa tunachumbiana - Ntalami.

• Tamko hili linajiri kipindi ambapo wengi wanahisi huenda anachumbiana na msanii Fena Gitu.

N
N
Image: Instagram

Mjasiriamali wa vipodozi Michelle Ntalami amewasuta vikali wanahabari na mablogu kwa kumnukuu vibaya katika mahojiano ya awali huku wakisema kuwa ana hulka ya kuwakataa wapenzi wake wa awali.

Kupitia ujumbe mrefu ambao Ntalami alilazimika kuweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, alisema kuwa wengi wamekuwa wakimnukuu vibaya, lakini akakubali kuwa uhusiano wake wa awali waliafikiana na mpenzi wake ambaye hakumtaja kuwa itakuwa ni siri na iwapo wangeulizwa kila mmoja angekanusha kabisa.

“Niliwahi kuwa kwenye uhusiano ambapo kutokana na asili yake na kutoaminiana sana ndani yake, sikujiamini kuithibitisha hadharani. Pia nilihisi kushinikizwa kusema tulivyokuwa kwenye vyombo vya habari. Tulikubaliana kwamba wakiuliza, ‘tutakataa.’ Jambo ambalo sote wawili tulifanya katika mahojiano, si mimi tu,” Ntalami alisema.

Mfanyibiashara huyo alisema kuwa mpaka leo hii anajuta kitendo hicho huku akisema kuwa angekuwa na uwezo wa kurudisha matukio nyuma basi hilo ni jambo ambalo asingelifanya kabisa.

Alisema kuwa katika safari yake ya mapenzi kwenda mbele, aliapa kutosema uongo na kueleza kila kitu kwa ukweli wake, akitolea mfano wa mahojiano ya hivi karibuni ambapo alilazimika kusema ukweli kuhusu uhusiano wake na msanii Fena Gitu.

Aliwasuta wale ambao wanamuona na marafiki zake wa kike na kiume na kuanza kueneza uvumi kuwa wanachumbiana. Alitaka hili likome mpaka pale mwenyewe atakapodhibitisha.

“Kusonga mbele, "binafsi lakini si siri" ni sera yangu. Nikifurahi kuongea juu ya maisha yangu ya uchumba, nitajibu kwa ukweli. Nina marafiki kadhaa wa kiume na wa kike. Ninaomba watu waache kudhani kuwa tunachumbiana au kuna mengi zaidi, kila mara ninapoonekana nao au tunaposhiriki matukio mtandaoni. Kisha ninapofafanua kwa ukweli, inaitwa ‘kukana.’ Acha. Hadi mimi mwenyewe nithibitishe uhusiano wangu, acha uvumi.”

Alisema kuwa wakati sahihi ukufika hawezi kumficha mpenzi wake na kama atakuwa na uhakika kwa asilimia mia kuwa ni mpenzi wake, hivyo kuwataka watu kukaa mkao wa kula na kusubiri tamko lake badala ya kueneza uvumi kuhusu maisha yake ya kimapenzi.

“Ninathamini amani yangu na faragha. Wakati utakapofika na nina uhakika wa 100% na mtu wangu, hakikisha kuwa haitakuwa siri. Wacha watu wawe. Acha yaliyopita yapumzike bila kuyaleta kila wakati ninapoonekana kuwa na furaha na kuendelea na maisha yangu,” Ntalami alifoka.