Otile Brown na Rayvanny waonekana kwenye studio, mashabiki watarajie collabo

Brown aliondoka nchini mapema wiki hii kwenda Tanzania ambapo alidokeza kuibiwa vipakatalishi katika uwanja wa ndege.

Muhtasari

• Endapo collabo yao itatoka, Otile atakuwa msanii wa kwanza kufanya collabo na wasanii wakubwa kutoka Tanzania akiwemo Alikiba, Harmonize na Jux.

Otile Brown na Rayvanny kutoa collabo
Otile Brown na Rayvanny kutoa collabo
Image: Instagram,

Msanii wa kizazi kipya kutoka Kenya Otile Brown huenda ziara yake nchini Tanzania mapema wiki hii ilikuwa ni kwa ajili ya maandalizi ya wimbo wake mpya akishirikiana na Rayvanny kutoka lebo ya Next Level Music.

Hili lilidhihirika baada ya Rayvanny kupakia video kwenye Instastory yake akiwa studioni na Otile Brown wakifanay maigizo ya kuimba wimbo.

Video hiyo pia ilipakiwa na Otile kwenye Instagram yake, lakini hakuna kati yao ameweka wazi iwapo wanatoa wimbo au la. Lakini dalili zote kwa asilimia kubwa zinaonesha huenda collabo ndio sababu yake kuu kuenda Tanzania.

Siku mbili zilizopita, msanii huyo wa Kenya alielekea Tanzania na kuweka mitandaoni kuwa jambo lisilo la kawaida liimtokea alipotua katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere.

Alisema kuwa watu wasiojulikana walimuibia vipakatalishi vyake viwili na hivyo kuipoteza furaha yake na kulemaza baadhi ya ratiba yake nchini humo.

Alipakia video akimwa mnyonge na kutoa ombi kwa yeyote ambaye angeweza kuvipata na kumrejeshea kuwa angempa zawadi nzuri na nono, huku akisema kuwa kompyuta hizo za mkononi zilikuwa na mambo mengi ya umuhimu mkubwa katika maisha yake ya Sanaa.

Baadae ni kama msamaria mwema alisikia kilio chake na kumrejeshea vipakatalishi vyake na Otile hakusita kuonesha furaha yake kwenye Instagram huku akisema kuwa kwa kweli ana mashabiki wengi ambao wanamkumbuka kwa Maombi ya kila dini.

Endapo hiyo collabo yake na Rayvanny itafanikishwa, basi msanii huyo ataingia kwenye vitabu kama msanii wa Kenya aliyefanya collabo na wasanii wengi wakubwa kutoka Tanzania.

Miaka miwili iliyopita alifanya collabo na Ali Kiba ambayo ilifanya vizuri kabla ya kurejea tena mwaka jana na kuachia collabo na wasanii Jux na nyingine na Harmonize ambazo zote zimefanya vizuri na muingiliano vya vina ukiwa wa kiwango cha ghorofani.