Jose Chameleone ampiga mijeledi mwanabodaboda, mkewe amshtumu hadharani

Katika video iliyoenezwa, Chameleone alishuka garini kabla ya kushusha kipigo kizito mgongoni mwa mhudumu huyo wa bodaboda.

Muhtasari

• Mwanabodaboda huyo alidaiwa kukwaruza Range Rover ya Chameleone kitendo kilichomfanya msanii huyo kugeuka mbogo.

Mkewe Chameleone amruka katika sakata la kumpiga mtu nyaunyo
Mkewe Chameleone amruka katika sakata la kumpiga mtu nyaunyo
Image: Instagram

Nchini Uganda hadithi kubwa ambayo imeenezwa pakubwa kwenye mitandao ya kijamii wikendi iliyopita ni kuhusiana na video iliyokuwa ikimuonesha msanii mkongwe Jose Chameleone akimtia mijeledi jamaa mwendesha bodaboda kwa kukwaruza gari lake aina ya Range Rover na pikipiki yake.

Watu walitoa maoni tofauti kufuatia tukio hilo ambalo lilitokea mwishoni mwa juma lililopita huku wengi wakionekana kukemea kitendo cha Chameleone.

Katika kile ambacho wengi hawakuwa wanatarajia, mkewe mwanamuziki huyo kwa jina Daniella Atimu, alionekana kukashfu kitendo hicho cha mumewe hadharani kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Atimu aliweka picha ya kukashfu kabisa vitendo vyovyote vya unyanyasaji huku akimlenga mumewe kwa kitendo cha kumpiga mwanabodaboda asiyekuwa na uwezo wa kujitetea.

Alidokeza waziwazi kuwa ako upande wa mwanabodaboda huyo kwa kutumia alama ya reli kuwa anahitaji kupata haki yake kwa kitendo cha kudhalilishwa na mumewe Jose Chameleone.

“Vita havina nafasi yoyote ya kuvumiliwa kokote kule. Haki na itendeke kwa mwendesha bodaboda mwathirika,” mkewe aliandika kwenye Instagram.

Awali, kisa hicho kilikuwa kimeibua maoni kinzani mitandaoni huku polisi wakilivalia njuga na msemaji wa mwanamuziki huyo alisema kuwa alilazimika kuchomoa nyaunyo na kumtandika kama mara tatu hivi mgongoni kwani mwendesha boda huyo baada ya kukwangura gari lake, alianza kuonesha jeuri badala ya kunyenyekea na kuomba radhi.

Alisema kuwa msanii wake alilazimika kutumia kiboko kama njia moja ya kujilinda kwani mhudumu huyo alikuwa anaongea maneno ya kumtishia vikali.