Tanasha Donna: Kila mtu anafaa kuoga mara tatu kwa siku

Mwanamuziki huyo alisema yeye hawezi kubaliana na wale wanaosema ‘mwanaume ni jasho’ huku akisema kudumisha usafi ni kwa watu wote.

Muhtasari

• "Usisahau kufanya utaratibu wa kukoga kati ya mara mbili na mara tatu kwa siku, piga mswaki, tumia kopo la msalani vizuri" - Donna.

Tanasha Donna azungumzia umuhimu wa kuoga
Tanasha Donna azungumzia umuhimu wa kuoga
Image: Instagram

Tanasha Donna amezungumzia kwa kina kuhusu umuhimu wa usafi wa mwili si tu kwa watu vwa jinsia ya kike bali kwa kila mtu anayependa ustaarabu.

Kupitia video fupi aliyoipakia Instagram, mwanamuziki huyo alifafanua kwa mapana jinsi watu wanafaa kusdumisha usafi katika miili yao na mazingira wanamoishi.

“Sijui ni mara ngapi tutalizungumzia hili lakini watu wangu, wanawake kwa wanaume, usafi ni kitu cha muhimu sana. Ni muhimu sana watu wangu kama hamkuwa mnajua,” Tanasha Donna alianza kushauri.

Alisema kuwa kwa mtu yeyote haijalishi unapitia changamoto gani katika maisha, lakini hakikisha unanukia vizuri popote uendapo, na si tu kwa kujipulizia marashi bali kwa kukoga mwili mara mbili hadi mara tatu kwa siku bila kusahau kupiga mswaki na kuvalia nadhifu muda wote.

“Hakikisha unanukia vizuri si tu kwa kujirembesha kwa marashi kwa nje, lakini usafi halali. Hakikisha unanawa mikono yako, usisahau kufanya utaratibu wa kukoga kati ya mara mbili na mara tatu kwa siku, piga mswaki, tumia kopo la msalani vizuri na pia osha kwa maji baada ya kumalzia kukata gogo. Nyoa nywele zote mwilini mwako, kaa nadhifu,” mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz alizungumza kwa msisitizo.

Alizidi mbele kunukuu kifungu maarufu kutoka kwa Biblia kinachosema kuwa usafi unamweka mtu karibu ya ucha Mungu akisema kuwa kama hakuna usafi karibu nawe, huwa unakosa hata utulivu wa akili.

“Natumai wengi wenu mmesikia nukuu kuwa usafi humweka mtu karibu na kumcha Mungu, ni ukweli watu wangu. Utagundua kuwa kukiwa na uchafu karibu nawe unapoteza dira ya akili lakini wakati kuna usafi unahisi mwenye utulivu na Amani. Miili yetu ni hekalu takatifu la Mungu, tuilinde wote wake kwa wanaume,” Alisema.

Vile vile, mwanamuziki huyo alisema yeye hawezi kubaliana na wale wanaosema ‘mwanaume ni jasho’ huku akisema kudumisha usafi ni kwa watu wote.