"Ni nini wewe!" Mwanahabari amkamata jamaa akijaribu kuingiza mkono mfukoni mwake (Video)

Mwanahabari huyo alikuwa anakusanya maoni ya watu katika uwanja wa Kamkunja wakati mmoja alimkaribia na kujaribu kumuibia.

Muhtasari

• Waandishi wa habari walikuwa wamekita kambi katika uwanja wa Kamkunji kusubiri kusikia tamko la Odinga kuhusu uchaguzi punde baada ya kurejea nchini kutoka SA.

Jumatatu kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga alirejea kutoka nchini Afrika Kusini alikokuwa akifanya ziara ya kimaendeleo kama mjumbe wa muungano wa Afrika kuhusu Miundombinu.

Odinga alirejea nchini kwa kishindo na kuelekea moja kwa moja katika uwanja wa Kamkunji jijini Nairobi ambapo wafwasi wake na wale wa Azimio walikuwa wamekongamana wakisubiri tamko lake kuhusu ufichuzi wa hivi majuzi kuhusu matokeo ya kura za Agosti mwaka jana.

Uwanjani Kamkunji, watu mbali mbali walikuwa wamekita kambi, wakiwemo wanahabari ambao walikuwa ange kunasa matukio hayo na kuchukua maoni ya baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo.

Video moja imeibuka mitandaoni ikimuonesha mwanahabari wa kituo cha runinga cha KBC ambaye alikuwa miongoni mwa watu akichukua maoni kabla ya mmoja wao kujaribu kumuingia mfukoni.

Katika video hiyo, mwanahabari huyo alikuwa anamsikiliza jamaa mmoja aliyekuwa akizungumza ni kwa nini alijitokeza katika mkutano huo wa kisiasa, kabla ya kijana mwingine kumkaribia na kufanya jaribio la kuingiza mkono wake mfukoni mwa ripota huyo.

Alichofanya ripota huyo ni kuruka kama mtu aliyetekenywa huku akiuliza swali la balagha kwa sauti iliyojawa na kero, “Ni nini wewe!” kabla ya klipu hiyo kutamatika.

Katika hotuba yake iliyosubiriwa na wengi, Odinga alisema kuwa za ndani kutoka IEBC zinaonesha kuwa alishinda uchaguzi huo na kuwa hawezi akamtambua rais Ruto na uongozi wake wowote.