Stephen Letoo afichua mada kuu ya Kongamano la wanaume siku ya Valentino

Letoo ni rais wa wanaume wenye wake wengi ukanda wa Afrika Mashariki na kati aliyejiteua mwenyewe.

Muhtasari

• Aliwarai wazazi wote kupunguza bei ya mahari ili kila mwanamume awe na uwezo wa kuoa wanawake zaidi ya mmoja.

letoo afichua mada kuu ya Men's Conference
letoo afichua mada kuu ya Men's Conference
Image: Facebook

Rais wa wanaume wenye wake wengi (mitala)  katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati Mwanahabari Stephen Letoo ametangaza kuwa anatafuta hela za kufanikisha ziara yake nchini Burkina Faso ili kufanya uchunguzi na kujifunza kuhusu suala la mwanamume kuwa na wanawake wengi kwa wakati mmoja.

Akizungumza na blogu moja ya humu nchini, Letoo alisema kuwa amevutiwa na taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo alisema ndilo linaongoza katika familia za wanaume wenye wake wengi katika bara la Afrika.

“Ninaenda kutafuta pesa ili nisafiri kwenda nchini Burkina Faso kwa sababu ni taifa ambalo linaongoza kwa mitala barani Afrika. Nataka tu kwenda kuangalia jinsi mambo yanafanywa kule na nitarudi na ripoti nzuri jinsi ya kuendesha familia zenye wake zaidi ya mmoja kwa njia ya ustaarabu,” Letoo alisema.

Letoo ambaye amekuwa akipigia debe pakubwa suala la kila mwanamume kuoa wanawake zaidi ya mmoja alisema kuwa ataendelea kusambaza ujumbe wa kuhimiza familia za wake wengi sio tu Afrika Mashariki bali pia kote Afrika.

Mwanahabari huyo pia aligusia mada kuu ya kongamano la wanaume, alilosema litafanyika sambamba na siku ya wapendanao ya Valentine. Alisema mada hiyo itajikita katika kurai na kuhimiza wazazi wa watoto wa kike kupunguza bei ya mahari ili kurahisishia kila mwanamume mzigo wa kuoa wanawake wengi.

“Mada kuu ya hiyo siku itakuwa ni kutoa wito kwa wazazi kupunguza bei ya mahari ili kuhakikisha wanaume wana uwezo wa kuoa wanawake wawili watatu au zaidi. Hilo tutalizungumzia kwa msisitizo mkubwa sana hiyo siku,” Letoo alisema.

MHARIRI:DAVIS OJIAMBO.