Bahati na Harmonize wazika tofauti zao, watimba studioni kufanya collabo

Bahati mwaka 2020 alimshambulia Harmonize mitandaoni akimtaka kuacha kulazimisha bifu na Diamond Platnumz.

Muhtasari

• Bahati atakuwa msanii wa tatu kutoka Kenya kufanya ushirikiano wa ngoma na Harmonzie baada ya Pipipili ya Willy Paul na Woman ya Otile Brown.

Harmonize na Bahati wako studioni kufanya collabo
Harmonize na Bahati wako studioni kufanya collabo
Image: Instagram

Msanii Bahati Kioko kutoka Kenya amefichua kwamba hatimaye huu ndio mwaka wa kufanikisha ndoto yake kwa kufanya collabo ya nguvu na mwenzake kutoka Tanzania, Harmonize.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bahati alipakia picha wakiwa pamoja na Harmonize huku akiisindikiza na maneno kuwa “2023, mko tayari kutupokea mimi na kakangu Harmonize?”

Harmonize naye alimwambia Bahati kwenye chapisho hilo kwa kumtaka amtumie kionjo cha ngoma hiyo wanayoshughulikia pamoja kupitia mtandao wa WhatsApp.

“Itume kaka kwenye ile namba yangu moja tu ya WhatsApp kaka nakukubali sana haijalishi nini. Sisi ni vijana wa mtaani,” Harmonize aliandika.

Bila Shaka iwapo Bahati atafanikisha collabo hii basi ataingia kwenye orodha kama ya msanii mwenzake Willy Paul kufanikisha kufanya collabo na wasanii Harmonize na Rayvanny kutoka Tanzania.

Wasanii hao wawili walionekana kutofautiana vikali miaka mitatu iliyopita pale ambapo Bahati alianza kumshambulia Harmonize kwenye mitandao wa Instagram akimtaka kutolazimisha bifu na aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.

Katika mashambulizi hayo yote, Harmonize alionekana kutomjibu lakini alienda mbele na kum-unfollow Bahati kinyemela.

Mwaka jana wawili hao walikutana nchini Uganda katika tamasha la kibabe la msanii Eddy Kenzo ambapo kupitia kwa msanii Bruce Melody kutoka Rwanda, walipatana na kuonekana wakisalimiana, hatua ambayo wengi walisema kuwa huenda wamezika tofauti zao.

Mashabiki wao wamewasihi kuachia dude hilo kwa haraka kwani ndio wanalisubiri kwa hamu mno.

Kwa upande wake Harmonize, Bahati atakuwa msanii wa tatu kutoka Kenya kufanya ushirikiano wa ngoma naye baada ya Pipipili ya Willy Paul na Woman ya Otile Brown.