"Masomo niliachia shule!" Trio Mio atupilia mbali uwezekano wa kujiendeleza kimasomo

Japo hakusema alama aliyoipata katika mtihani wa KCSE, Trio Mio aliweka wazi kuwa alifurahia kile alichopata.

Muhtasari

• Msanii huyo sasa amefunga milango yote ya masomo na fikira zote ziko kwenye taaluma yake ya muziki.

Msanii Trio Mio azungumza kuhusu mipango yake.
Msanii Trio Mio azungumza kuhusu mipango yake.
Image: Screengrab

Msanii rapa mchanga wa humu nchini Trio Mio amezungumza kuhusu hatma yake katika Nyanja za masomo baada ya kumaliza kidato cha nne katika mtihani wa KCPE wa mwaka jana.

Awali msanii huyo alikuwa amesema kuwa alikuwa na nia ya kujiendeleza kimasomo katika kitivo cha ubunifu lakini ni kama amebadili nia yake akisema kuwa hafikirii kuendelea na masomo Zaidi ya sekondari tu.

Katika mahojiano na mwanablogu mmoja, Mio alisema kuwa kwa sasa anafikiria jinsi ya kujiboresha Zaidi katika muziki wake na pia kuwaunganisha vijana wenzake kupata ajira, huku akisema kuwa suala la masomo lina wenyewe na yeye hafikirii kuwa mmoja wao.

“Mimi kando na muziki, kuna biashara zingine ninafanya. Kwa mfano nataka kuwakimu vijana kupata ajira. Suala la masomo hilo Nimeachia shule lakini ningependa kufanya kozi ya ubunifu  huko mbeleni ila kwa sasa nataka kujikita Zaidi katika muziki na biashara zangu,” Trio Mio alisema.

Matokeo ya mtihani wa kitaifa wa shule za sekondari KCSE yalitolewa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu mwezi mmoja uliopita na baadhi walifurika kwenye mitandao wakidai kujua alama aliyopata msanii huyo aliyekuwa miongoni mwa watahiniwa.

Hata kama Trio Mio mwenyewe hakuweka wazi alama aliyopata, baadhi walizua kuwa alianguka kwa kupata alama ya D huku wengine wakisema alipata E, lakini katika mahojiano hayo, Mio alisema kuwa yeye binafsi alifurahia na kujikubali kile alichokipata katika KCSE.

Mama yake ambaye ndiye meneja wake alikanusha kipindi hicho kuwa uvumi wa mwanawe kupata D ulikuwa wa kupotosha huku naye pia akigoma kabisa kusema alama mwanawe alipata.