Lilian Ng'ang'a: Matamshi ya Linet Toto kuhusu Odinga yananipa wasiwasi naye

Ng'ang'a alidokeza kwamba mbunge huyo wa kaunti alitumia uhuru wake wa kuzungumza hadharani vibaya.

Muhtasari

• Toto alifaa kujishughulisha za siasa za mashinani na suala la siasa za kitaifa kuachia wanasiasa waliokuwa kwenye tasnia hiyo kwa muda.

Lilian Ng'ang'a amkosoa Toto kwa kumshambulia Odinga.
Lilian Ng'ang'a amkosoa Toto kwa kumshambulia Odinga.
Image: Maktaba, Twitter

Aliyekuwa mke wa gavana wa kwanza wa Machakos Alfred Mutua, Lilian Ng’ang’a amekuwa mtu wa hivi karibuni kujitosa kwenye gumzo la siasa akitoa maoni yake kuhusu matamshi ya mwakilishi wa kike wa Bomet Linet Chepkorir almaarufu Toto.

Toto amekuwa akizungumziwa kwa njia mseto na watu mitandaoni baada ya video kuibuka akimkejeli na kukashifu kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.

Katika video hiyo, Toto na viongozi wengine kutoka eneo la Bonde la Ufa walikuwa wamehudhuria hafla ya kutoa shukrani ya mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek.

Mbunge huyo wa kaunti ya Bomet mwenye umri mbichi alimshambulia Odinga akisema kuwa alianza siasa zake hata kabla hajazaliwa na mpaka sasa hivi wakati amekua na kuchaguliwa kama kiongozi, bado siasa za Odinga hazijawahi isha.

Watu wamekuwa wakizungumza yao mitandaoni na Ng’ang’a pia ametoa tamko lake akielekeza bomu kwa Toto.

Ng’ang’a ambaye alijiondoa kwenye ndoa yake na gavana Mutua mwezi Oktoba mwaka 2021 alimshauri Toto kuwa licha ya uwepo wa uhuru wa kuzungumza lakini mambo mengine kama kiongozi anayejitambua hafai kuzungumza.

“Uhuru wa kujieleza ndio lakini hii inanifanya niwe na wasiwasi, binti mdogo,” Ng’ang’a aliandika kwenye retweet ya matamshi ambayo mbunge huyo wa kaunti alinukuliwa akisema.

Mjadala huo unaendelea kushika kasi huku mbunge Salasya pia akijikuta katika zogo lenyewe kwa kusema kuwa dawa ya Toto ni kumpachika mimba.