Moya David: Ukiiga mtindo wa densi yangu nakuchukulia hatua za kishera

Ni ubunifu wangu lakini watu wakati mwingine hawanipi utambuzi unaonifaa. - Moya David.

Muhtasari

• Nilifanya hivyo kwa sababu ni mtindo ambao ninakuja nao kiasili na wakati mwingine naona watu wanautumia vibaya ndio maana nilichukua hati miliki. - Moya David.

Moya David, mcheza densi.
Moya David, mcheza densi.
Image: Moya David//Instagram

Mcheza densi Moya David amefichua kwamba amechukua hati miliki kwa mtindo wake wa kucheza densi anapowasilisha zawadi kwa watu ambao anatumwa kuwashtukizia na zawadi.

 

Akizungumza Jumanne wakati wa kuzindua saluni yake mpya Kitengela, David alisema kwamba alilazimika kuchukua hati miliki kwa densi zake kwa sababu kwa muda mrefu amekuwa akiona watu jinsi wanaichafua na wengine wanaiga bila hata kumtambua kuwa ndiye muasisi wa densi ya aina hiyo.

 

“Nimechukua hati miliki za Moya David na sasa hivi mpaka mtindo wangu wa kucheza densi nimeuchukulia hati miliki. Nilifanya hivyo kwa sababu ni mtindo ambao ninakuja nao kiasili na wakati mwingine naona watu wanautumia vibaya ndio maana nilichukua hati miliki. Ni ubunifu wangu lakini watu wakati mwingine hawanipi utambuzi unaonifaa. Mtu yeyote ambaye atajaribu kuiga mtindo wangu sheria itachukua mkondo wake. Mitindo yote ya densi ambayo ninafanya nimeichukulia hati miliki,” Moya David alisema.

 

Wengi walihisi Moya kutamka wazi wazi kwamba atachukua sheria dhidi ya watakaoiga mitindo yake ni kumlenga mkuza maudhui Trevor Silaz ambaye pia anafanya sawa kama Moya kutoka kucheza densi hadi utepe mweupe anaoufunga kichwani.

 

Mkuza maudhui huyo kwenye mtandao wa Tiktok pia alitoa onyo kali kwa wale wote ambao wanaendesha akaunti ghushi kwenye mitandao ya kijamii wakijifanay kuwa ni yeye ili kuwarubuni na kuwalaghai Wakenya.

Japo hakutaja hatua atakazowachukulia, David alisema siku yao itafika watakiona cha mtema kuni.