Jalang'o afurahi kukutana na rafiki waliyefanya kazi ya kuuza mikate naye mwaka 2001

Mbunge huyo wa Lang'ata alisimulia jinsi alivyokuwa akichuuza mikate kwa baiskeli miaka ya 2000 walikokutana na rafiki yake.

Muhtasari

• Mbunge huyo alisimulia jinsi alikuwa kiguu na njia katika vichochore vya mji wa KItale kutafuta wanunuzi w bidha hiyo.

• Alikuwa akizungusha mikate kwa kutumia baiskeli na walikuwa wanashirikiana na rafiki yake kupika.

Mbunge wa Lang'ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang'o ambaye alikuwa mwigizaji katika kipindi cha Papa Shirandula na pia mtangazaji, aliweka wazi furaha yake kukutana na rafiki yake wa zamani kwa jina Phillo Oyamo ambaye walikuwa naye katika mji wa Kitale.

Jalang'o alisema kwamba imekuwa zaidi ya miaka ishirini tangu walipoonana naye. Mbali na hiyo,alieleza safari yake mjini Kitale kabla ya kufanikiwa kwake.

Alieleza jinsi wakati mmoja baada ya kuelekea likizoni baada ya shule, alialikwa na shangazi yake mjini Kitale ili kufanya masomo ya ziada katika shule ya Central Primary. Phillo alikuwa ndiye msimamizi wa duka la shangazi yake la kuoka na kuuza mikate.

Mcheshi huyo alikumbuka jinsi walikuwa wanaamka saa kumi alfajiri jogoo la kwanza kwa ajili ya kuandaa mapishi ya mikate.

Alisema kwamba anaujua mji wa Kitale ndani na nje kama kiganja chake kwani vichochoro vyote ndiko alikokuwa akizunguka na baiskeli yake kutwa nzima akichuuza mikate hiyo mapema miaka ya 2000.

Mbunge huyo ambaye kama mtu mwingine yeyote asiyekuwa na msaada wa mtu mwenye ushawishi wa kumhakikishia kazi nzuri alipitia safari ya milima na mabonde hadi kufikia kiwango alicho nacho hivi sasa.

Kwa wakati mmoja, aliwahi kushiriki kama muigizaji wa vitabu vya shule za upili kabla ya kujiunga na ucheshi baada ya biashara ya kuchuuza samaki katika ufuo wa ziwa Victoria kugonga mwamba.

Kupitia ucheshi, alipata nafasi kuingia kwenye redio kama mmtangazaji mwenza wa zamu na umaarufu wake ukazidi kukwea hadi mwaka jana alipogura na kujitosa kweye siasa kuwania ubunge Lang'ata.

Kwa bahati nzuri, aliibuka mshindi kupitia tikiti ya chama cha ODM akimbwaga aliyekuwa mbunge Nixon Korir aliyejaribu kutetea kiti hicho kupitia chama cha UDA bila mafanikio.