Karangu Muraya: Waniuliza naendelea aje kumbe ndio wananiombea mabaya

Muraya alipakia picha akiwa hospitalini huku watu mbalimbali wakimtembelea na kumtakia nafuu ya haraka.

Muhtasari

• “Watu wale wale ambao wananiuliza shinikizo la damu liko aje ndio hao hao walionipangia mabaya." - Muraya.

Karangu Muraya akiwa hospitalini.
Karangu Muraya akiwa hospitalini.
Image: Facebook.

Siku moja iliyopita, Karangu Muraya alidokeza kwamba alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua.

Mfadhili huyo ambaye amejizoea umaarufu kutokana na vitendo vyake vya kunyoosha mkono wa msaada kwa watu wenye shida na matatizo ainati sasa ameibuka na mapya kwamba kuna baadhi ya watu wanaojijongeza karibu naye kujifanya wanamuombea afueni ya haraka kumbe nyuma ya mgongo wake ndio hao hao wanaomuombea mabaya.

Muraya alipakia picha akiwa katika kitanda cha hospitali na kuwaomba wenye mioyo safi kumkumbuka katika dua huku akiwakashfu wale aliowataja kama “wenye roho mbaya” ambao wanamuombea mabaya.

“Watu wale wale ambao wananiuliza shinikizo la damu liko aje ndio hao hao walionipangia mabaya. Mungu tafadhali niponye,” Karangu alisema.

Watu wengi wanaoshabikia kazi yake nzuri katika juhudi za kuibadilisha jamii kwa kuweka tabasamu kwenye nyuso za kila mmoja walifurika kwenye chapisho hilo wakimtakia kupona kwa haraka.

“Mungu akufiche kabisaa... Mola aiondoshee mitego yote... Nkt..!!” Lizbett Gachuh alisema.

“Acha Kufikiria juu kupita kiasi. Wewe ni mtu mkuu wa Mungu. Waombee. Pona na endelea na kazi nzuri,” Simon Gatheru alimwambia.

“Wewe sio mgonjwa ni ishara tu ya kuwaonyesha adui zako Mungu Anakupenda na Kukulinda, kumbuka Ayubu ambaye hata mke alimwambia kumtukana Mungu.Wewe ni mshindi.utafanikiwa kwa Jina Kuu la Yesu Kristo,” Esther Njoroge.