Willy Paul:Sitaki kushiriki mapenzi, nimechagua kuwa mtakatifu kabisa

Msanii huyo pia aliwataka wanawake kumpa wakati rahisi kwa kutompa majaribu na vishawishi.

Muhtasari

• Kwa muda mrefu, Willy Paul hajawahi mtambulisha hadharani mpenzi wake.

• Katika miaka 2 iliyopita, Diana Marua na Miss P walijitokeza na madai kwamba msanii huyo aliwahi fanya jaribio la kuwadhulumu kingono.

Msanii Willy Paul asema ana mpango wa kubaki mseja
Msanii Willy Paul asema ana mpango wa kubaki mseja
Image: Instagram

Msanii Willy Paul ametangaza kuwa ana mradi mkubwa sana unakuja na ili kuufanikisha kwa viwango vikubwa, amefanya uamuzi wa kusalia bila mpenzi kwa kipindi chote.

Msanii huyo ambaye alipokezwa tuzo ya dhahabu na YouTube kwa kufikisha wafuasi milioni moja alisema kuwa anataka kuwa mseja na hivyo kuwataka wanawake kufanikisha hilo kwa kutompa majarida ambayo huenda yatamtumbukiza kwenye kushiriki mapenzi tena.

“Nitabaki kubaki mseja Ili Tukio Langu Linalokuja Lifanikiwe... Nachagua Kuwa Mtakatifu Kabisa... wanawake tafadhali Nifanyie Rahisi Mchakato Huu. Asante Kwa Kunielewa,” Pozee alitoa ombi kwa kina dada.

Willy Paul alipokezwa tuzo hiyo ya dhahabu ambayo mtandao wa YouTube aghalabu hutoa kwa watumizi wake ambao wamefikisha idadi kubwa ya wafuasi, na alijipiga kifua akitamba kwamba nchini ndiye msanii wa pekee ambaye ana ufuasi halali ambao si wa kurubuni.

Aliwasuta baadhi ya wanablogu waliozua kuwa wafuasi wake wengi walikuwa hewa baada ya kufikisha milioni moja miezi kadhaa iliyopita.

Pozee alifafanua kwamba alifikisha milioni moja lakini hakutuma ombi rasmi kwa YouTube kumpa zawadi hiyo.

“Ningependa kuwashukuru sana wafuasi wangu, tumefika milioni moja YouTube nah ii hapa ni tuzo. Sababu imenifanya niwataarifu hili ni kutokana na mwanablogu Fulani aliyetangaza mitandaoni eti ufuasi wangu ni wa kimchongo YouTube. Nilifikisha ufuasi wa milioni moja kwenda mbele miezi kadhaa iliyopita, ila sikutoa ombi kwa YouTube kwa ajili ya zawadi hii. Katika hii nchi yote tunajua kuwa Willy Paul ndiye ako na takwimu halali, mnajua hivyo nyote…” Pozee alijitapa.

Msanii huyo kwa muda mrefu hajawahi kumtambulisha hadharani mpenzi wake, haswa baada ya miaka miwili iliyopita mwanablogu Diana Marua kufanya video akilia na kumtuhumu Pozee kwa jaribio la kumnyanyasa kingono.

Pozee aliwahi mahakamani na kumshtaki Marua katika kile alisema ni “kuchafuliwa jina” na kuitaka mahakama kumshrutisha Marua kuiondoa video ile, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.