"Ni uongo huo!" Simple Boy akanusha kumuiga Khaligraph kwenye wimbo wake mpya

Katika wimbo mpya wa "Inabamba", Wengi wamekuwa wakihisi Simple Boy aliiga wazo la Khaligraph kwenye wimbo wake wa "Kwame"

Muhtasari

• Stevo alisema anazidi kupambana kivyake kuhakikisha anakwea kweney viwango vya juu kama wenzake.

• Hata hivyo, alibainisha kuwa waongozaji wa video yake na ile ya Khaligraph wote wanatoka Tanzania.

STEVO AKANUSHA KUMUIGA KHALIGRAPH.
STEVO AKANUSHA KUMUIGA KHALIGRAPH.
Image: INSTAGRAM

Siku mbili zilizopita, msanii Stevo Simple Boy aliachia wimbo wake mpya kwa jina ‘Inabamba’ na baadhi ya watu wamekuwa wakizua kwamba aliiga na kuiba mtindo wa msanii wa kufoka Khaligraph Jones katika moja ya wimbo wake.

Wimbo wa Stevo unakaribiana kwa kiasi kikubwa na wimbo wa Khaligraph aliomshirikisha Harmonize wiki mbili zilizopita kwa jina ‘Kwame’ – haswa katika mazingira ambayo video zilifanywa.

Stevo hata hivyo baada ya kufikiwa na madai hayo, ameamua kutema nyongo na kuweka wazi kwamba hakuiba wazo na video ya Khaligraph hata kidogo licha ya ukweli kuwepo kuwa waongozaji wa video zote mbili wanatoka katika taifa jirani la Tanzania.

“Wengi wanasema nimeiga Khaligraph katika video yangu mpya ya Inabamba, ila ningependa kusema kuna utofauti mkubwa san ahata kama waongozaji waliofanya hizo video zote mbili wanatoka Tanzania,” Stevo alisema.

Aliweka wazi kwamba yeye yuko makini na kazi yake asili na wala hayupo kwenye Sanaa ya muziki wa Kenya kwa ajili ya kuiga na kuiba mawazo ya wasanii wenzake.

 Msanii huyo kutoka Kibera alionesha nia yake ya kupambana kivyake katika Sanaa pana ya muziki ili kufika kwenye viwango vya juu kama wengine ambao anaambiwa anawaiga.

“Mimi nipo tu nafanya kazi zangu na sina nia ya kumuiga mtu yeyote ila napambana sana pia kufika viwango vya juu kisanii na naahidi mambo makubwa yanakuja yenye utofauti na pia jinsi yangu ya kuimba itabadilika sana,” Stevo aliwaahidi mashabiki wake.

 Msanii huyo alimaliza kwa kutoa zake shukrani za dhati kwa mashabiki wote wanaompa sapoti tangu siku ya kwanza mwaka 2019 alipotusua kwenye Sanaa na kibao maarufu ya Mihadarati.