Kwa mara ya kwanza Nyashinski kusababisha kwenye jukwaa moja na Les Wanyika

Tamasha la Blankets & Wine litafanyika Aprili tarehe mbili katika bustani ya Laurete ndani ya Uwanja wa Kasarani.

Muhtasari

• Mashabiki wengi wameonesha utayarifu wao kushuhudi historia ikiandikishwa wakati Les Wanyika watakipiga kwenye jukwaa moja na Nyashinski.

Nyashinski kukipiga kwenye jukwaa moja na Les Wanyika.
Nyashinski kukipiga kwenye jukwaa moja na Les Wanyika.
Image: Facebook

Kwa mara ya kwanza Kenya itashuhudia tamasha la aina yake katika ukumbi mdogo wa uwanja wa Kasarani mnamo Aprili tarehe 2 mwaka huu wakati msanii Nyashinski atakipiga mubashara jukwaani na bendi maarufu ya muda mrefu katika miziki ya Rhumba, Les Wanyika.

Tamasha hiyo kwa jina Blankets & Wine ambalo linaandaliwa na Muthoni Drummer Queen litakuwa la aina yake na maandalizi yanaendelea vyema ambapo sasa imebainika Nyashinski atatumbuiza kwenye jukwaa moja na Les Wanyika katika tamasha la kihistoria.

“Tunaiweka kuwa ya Kenya tu! Kuanzia Nyashinski hadi Les Wanyika, pata wasanii wote uwapendao wa Kenya kwenye jukwaa la Blankets & Wine katika Laurete Gardens, Uwanja wa Kasarani tarehe 2 Aprili. Tikiti zinapatikana sasa kwenye bio yetu,” taarifa hiyo ilisoma.

Tamasha la Blankets & Wine linatarajiwa kufanyika mara nne kwa mwaka huu pekee huku tarehe 2 Aprili ikiwa ni awamu ya kwanza.

Awamu ya pili itafanyika mwezi Julai, la tatu mwezi Oktoba na la mwisho kufunga mwaka mwezi Desemba kulingana na taarifa kutoka kwa Muthoni Drummer Queen, muasisi wa tamasha hilo.

Kulingana na waandalizi, mwaka huu, wanapanga kuandaa matoleo manne ya tamasha hilo kila Jumapili ya kwanza ya kila robo mwaka na Jumapili ya mwisho kabla ya Krismasi katika Bustani ya Laurete, ndani ya Home of Heroes, uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi, Kasarani.

Msanii wengine watakaotumbuiza katika hafla hiyo ya Aprili 2 ni pamoja na Boutross, Xenia Manasseh, Lisa Oduor, Okello Max na Kinoti.