Naomba mke mwema lakini napata 'single mother' - Ommy Dimpoz ataja sababu ya kutooa!

Msanii huyo alitaja tatizo hilo kama la "kiufundi" kote duniani kwa kila mwanamume anayetafuta mke mwema.

Muhtasari

• Kwa kauli yake, huenda hili ndilo tatizo ambalo kwa muda limekwamisha juhudi zake za kupata mchumba.

Ommy Dimpoz ataja sababu ya kutooa
Ommy Dimpoz ataja sababu ya kutooa
Image: Instagram

Msanii Ommy Dimpoz anahisi kwamba kuna tatizo la kiufundi kote duniani haswa ikija ni maswala ya wanaume kuomba au kutafuta wanawake wazuri wa kutulia nao katika ndoa.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 35 bila kiashiria chochote cha mke wala mtoto hata yule wa kusingizwa aliandika haya kupitia ukurasa wake wa Snapchat akisema kwamba wanaume wengi wamekuwa wakilipata tatizo hilo la “kiufundi” ambapo wanaomba wake wema wa kuoa lakini wanachokipata ni kina mama waliozaa na hawana wanaume.

“Sasa hivi kuna tatizo la kiufundi duniani, yaani ukiomba mke mwema unaletewa singo maza,” Ommy Dimpoz aliandika akimalizia na emoji za kucheka.

Ommy Dimpoz kwa muda amekuwa akikwepa kuzungumzia kuoa na kinachojulikana kumhusu ni mpenzi wake Maya Mia aliyefariki miezi kadhaa iliyopita, japo pia aliweka wazi kwamba walikuwa wameachana naye muda mrefu tu.

Mia alifariki katika hali ambayo haikuwekwa wazi lakini Dimpoz alikuwa mstari wa mbele kuongoza waombolezaji wengine kumuomboleza mrembo huyo.

Kwa kauli yake, huenda hili ndilo tatizo ambalo kwa muda limekwamisha juhudi zake za kupata mchumba kwani huenda amekuwa akijaribu kumtafuta mke mzuri na mwema wa kumzalia lakini anaowapata ni wale waliozaa na hawana wanaume, kwa kimombo ‘single mothers’

Lakini hayuko peke yake, wasanii wengi tu waliofanikiwa kumuziki wameshindwa kupata wake wazuri wa kuishi nao licha ya kuwa na umri mzuri wa kuingia kwenye ndoa.

Alikiba alijaribu hadi kufunga ndoa ya Kiislamu na mrembo kutoka Kenya lakini ndoa yake iliota mabua na kumalizia kusambaratika licha ya msanii huyo msiri wa mambo ya kibinafsi kuwa kimya kuhusu hilo muda wote huu.

Wasanii wengine kina Diamond, Harmonize, Rayvanny pia hawajawa na bahati kwani wamekuwa katika mahusiano mbalimbali lakini hakuna tija wamepata.