Zuwena atumia mapato kutoka kwa Diamond kutoa msaada wa chakula kwa yatima

Zuwena alisema kwamba Diamond alimlipa milioni 17 za Kenya kucheza kama vixen kwenye video ya wimbo wake wa "Zuwena"

Muhtasari

• “Sadaka ya thabiti ni kwa yatima, wenye uhitaji na wajane..” mmoja alimwambia.

Zuwena wa Diamond akitoa msaada wa chakula
Zuwena wa Diamond akitoa msaada wa chakula
Image: Instagram

Vixen wa video ya Diamond Platnumz, Zuwena ambaye jina lake halisi ni Recho Elias amegusa mioyo ya watoto mayatima baada ya kuwatembelea na kuwapa msaada wa bidhaa mbalimbali, nyingi zikiwa ni chakula.

Mwanadada huyo aliyetamba baada ya kuigiza kama Zuwena kwenye video ya Diamond aliyoiachia mwezi jana, mpaka wengi kumpa jina la Zuwena kabisa alipakia picha hizo akiwapa chakula watoto hao kwa furaha.

Kutoka kwa picha hizo, Zuwena alikuwa katika kituo kimoja cha kulelea watoto yatima kwa jina Maunga, Kinondoni nchini Tanzania na aliandamana na baadhi ya watu waliokwenda kumsaidia kugawanya msaada wake kwa watoto hao.

Mrembo huyo alisema kwamba siku zote mapenzi yake kwa watoto yatima yatasalia kuwa asilimia mia kwa mia wala hayawezi punguka.

Mapenzi yangu kwa watoto yatima 100%♥️🙏"”Zuwena aliandika.

Mashabiki wake walimpongeza kwa kunyoosha mkono wa fadhila kwa jamii wakimtaka kutokoma kufanya mema ili kupata thawabu.

Sadaka ya thabiti ni kwa yatima, wenye uhitaji na wajane..” mmoja alimwambia.

“Safi sana Zuwena jambo jema hili na wengine tunapaswa kufanya kuiga mfano,” Alex Ndagile aliandika.

Zuwena aliwahi kusema kwamba shukrani zake na mafanikio makubwa ya maisha yake muda wote zitaenda kwa msanii Diamond kwa kumtoa kimaisha, akisema kwamba kwa kucheza kama vixen kwenye wimbo wa Zuwena tu, alilipwa milioni 17 pesa za Kenya.

Hata hivyo, aliwahi zua ukakasi mitandaoni kwa kudai kwamba umri wake ni miaka 17, jambo ambalo wengi walipinga vikali wakimtaka kuacha masihara.