Trio Mio: Kwa nini sikuweka wazi matokeo yangu ya KCSE

"Maisha ni yangu na najua niko vizuri katika kile ninachokifanya," - Trio Mio.

Muhtasari

• Achene hizo, mimi hamkunijua juu ya darasa bali juu ya muziki - Trio Mio alisema.

Image: INSTAGRAM// TRIO MIO

Msanii wa kizazi kipya Trio Mio amefunguka sababu zake za kutoweka wazi matokeo yake ya mtihani wa kitaifa wa KCSE mwezi Januari.

Katika mahojiano ya kipekee ya mwanablogu Nicholas Kioko, Mio alisema kwamba ni wakati Wakenya wajishughulishe na masuala yanayowahusu na kukoma kufuatilia mambo ya wengine.

Alisema kwamba haikuwa lazima kwa kila shabiki wake kujua alipata alama gani kwani wote hawakumjua kwa sababu ya masomo bali walimjua kwa sababu ya muziki wake.

“Mimi sikukataa kuweka wazi kaka, watu washughulike na maisha yao, kwani wanadai kunilipia karo ya chuo kikuu. Achene hizo, mimi hamkunijua juu ya darasa bali juu ya muziki na najua niko vizuri katika kile ambacho ninakifanya. Maisha ni yangu,” Trio Mio alisema.

Msanii huyo mchanga alikuwa miongoni mwa wanafunzi wengi waliofanya mtihani wa KCSE mwaka jana na waziri wa elimu Ezekiel Machogu alipotangaza matokeo hayo mapema mwaka huu, mitandao ya kijamii ilivuma kwa madai kila mmoja akitaka kujua msanii huyo alipata alama ani.

Baadhi walikisia kwamba alifeli vibaya ndio maana hakuona haja ya kuwatangazia mashabiki wake huku wengine wakisema kwamba alipata alama za juu.

Baadae alisema kwamba angefanya kosi ya ubunifu katika chuo kikuu lakini mwezi jana katika mahojiano mengine, Mio alisema kwamba hana ndoto ya kuendelea na msomo tena, kwani alikofikia tayari ametosheka.

Mimi kando na muziki, kuna biashara zingine ninafanya. Kwa mfano nataka kuwakimu vijana kupata ajira. Suala la masomo hilo Nimeachia shule lakini ningependa kufanya kozi ya ubunifu  huko mbeleni ila kwa sasa nataka kujikita Zaidi katika muziki na biashara zangu,” Trio Mio alisema.